Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 32:22-33 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Uliwapa nchi hii ambayo uliahidi kuwapa wazee wao, nchi inayotiririka maziwa na asali.

23. Nao walifika, wakaitwa na kuimiliki. Lakini wao hawakukusikiliza, wala hawakufuata sheria zako. Hawakutenda mambo uliyoamuru. Ndiyo maana utawafanya wapatwe na balaa hii.

24. Tazama, Wakaldayo wamechimba mahandaki kuuzunguka mji; wameuzingira ili wapate kuuteka; wanaushambulia. Vita, njaa na maradhi vitaufanya mji utekwe na watu hao. Kweli mambo uliyotabiri yametokea. Unaona mwenyewe.

25. Lakini, ee Mwenyezi-Mungu, wewe ndiwe uliyeniambia: “Nunua shamba kwa fedha na kuweka mashahidi,” ingawa mji wenyewe umetekwa na Wakaldayo.

26. Ndipo Mwenyezi-Mungu akaniambia,

27. “Tazama, mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa watu wote. Hakuna lolote linaloweza kunishinda.

28. Kwa hiyo, mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Ninautoa mji huu kwa Wakaldayo na kwa Nebukadneza mfalme wa Babuloni, naye atauteka.

29. Wakaldayo wanaoushambulia mji huu wataingia na kuuchoma moto; watauteketeza pamoja na nyumba ambazo juu ya paa zake ubani ulifukiziwa mungu Baali na tambiko za divai zilimiminiwa miungu mingine, ili kunichokoza.

30. Maana Waisraeli na watu wa Yuda hawakufanya chochote mbele yangu isipokuwa uovu tangu ujana wao; watu wa Israeli hawakufanya chochote isipokuwa kunikasirisha kwa matendo yao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

31. Mji huu umechochea hasira yangu na kuniudhi tangu siku ulipojengwa mpaka leo hii. Kwa hiyo, nitautoa kabisa mbele yangu,

32. kwa sababu ya uovu wote waliotenda watu wa Israeli na watu wa Yuda, pamoja na wafalme na viongozi wao, makuhani na manabii wao, na wakazi wa Yerusalemu.

33. Wao walinipa kisogo badala ya kunigeuzia nyuso zao; ingawa nimewafundisha tena na tena, wao hawakusikiliza na kuyapokea mafundisho yangu.

Kusoma sura kamili Yeremia 32