Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 31:8-24 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Tazama, nitawaleta kutoka nchi ya kaskazini,nitawakusanya kutoka miisho ya dunia.Wote watakuwapo hapo;hata vipofu na vilema,wanawake waja wazito na wanaojifungua;umati mkubwa sana utarudi hapa.

9. Watarudi wakiwa wanatoa machozi,nitawarudisha nikiwafariji;nitawapitisha kando ya vijito vya maji,katika njia iliyonyoka ambamo hawatajikwaa;maana mimi nimekuwa baba wa Israeli,Efraimu ni mzaliwa wangu wa kwanza.

10. Enyi mataifa, sikilizeni neno langu mimi Mwenyezi-Mungu,litangazeni katika nchi za mbali,semeni: ‘Aliyemtawanya Israeli, atamkusanya,atamtunza kama mchungaji atunzavyo kondoo wake.’

11. Maana mimi Mwenyezi-Mungu nimemkomboa Yakobo,nimemwokoa kutoka kwa wenye nguvu kuliko yeye.

12. Watakuja na kuimba kwa sauti juu ya mlima Siyoni,wataona fahari juu ya wema wangu mimi Mwenyezi-Mungu,kwa nafaka, divai na mafuta niwapavyo,kwa kondoo na ng'ombe kadhalika;maisha yao yatakuwa kama bustani iliyotiliwa maji,wala hawatadhoofika tena.

13. Ndipo wasichana wao watafurahi na kucheza,vijana na wazee watashangilia kwa furaha.Nitageuza maombolezo yao kuwa furaha,nitawafariji na kuwapa furaha badala ya huzuni.

14. Nitawashibisha makuhani kwa vinono,nitawaridhisha watu wangu kwa wema wangu.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

15. Mwenyezi-Mungu asema hivi:“Sauti imesikika mjini Rama,maombolezo na kilio cha uchungu.Raheli anawalilia watoto wake,wala hataki kufarijiwa kwa ajili yao,maana wote hawako tena.

16. Sasa, acha kulia,futa machozi yako,kwani utapata tuzo kwa kazi yako,mimi Mwenyezi-Mungu nimesema;watoto wenu watarudi kutoka nchi ya maadui zenu.

17. Yapo matumaini kwa siku zenu zijazo,mimi Mwenyezi-Mungu nimesema;kwani watoto wenu watarejea nchini mwao.

18. “Nimesikia Efraimu akilalamika:‘Umenichapa ukanifunza nidhamu,kwani nilikuwa kama ndama asiyezoea nira.Unigeuze nami nitakugeukia,kwani wewe ndiwe Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu.

19. Maana baada ya kukuasi, nilitubu,na baada ya kufunzwa, nilijilaumu,nikaona haya na kuaibika,maana lawama za ujana wangu ziliniandama.’

20. “Efraimu ni mwanangu mpendwa;yeye ni mtoto wangu nimpendaye sana.Ndio maana kila ninapomtisha,bado naendelea kumkumbuka.Moyo wangu wamwelekea kwa wema;hakika nitamhurumia.Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

21. “Weka alama katika njia zako,simika vigingi vya kukuongoza,ikumbuke vema ile njia kuu,barabara uliyopita ukienda.Ewe Israeli rudi,rudi nyumbani katika miji yako.

22. Utasitasita mpaka liniewe binti usiye mwaminifu?Maana, mimi nimefanya kitu kipya duniani:Mwanamke amtafuta mwanamume.”

23. Mwenyezi-Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi: “Nitakapowafanikisha tena watu wa Israeli, wao watatangaza tena katika nchi ya Yuda na katika miji yake wakisema:‘Mwenyezi-Mungu akubariki ewe makao adili,akubariki ee mlima mtakatifu!’

24. “Ndipo watu wa Yuda na miji yake yote, wakulima na wachungaji wanaopitapita na makundi yao, watakaa huko pamoja.

Kusoma sura kamili Yeremia 31