Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 31:32-40 Biblia Habari Njema (BHN)

32. Agano hili halitakuwa kama lile nililofanya na wazee wao nilipowatoa kwa mkono wangu kutoka Misri; agano hilo walilivunja, ingawa mimi nilikuwa Bwana wao. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

33. Baada ya siku hizo, nitafanya agano lifuatalo na Waisraeli: Nitaiweka sheria yangu ndani yao, na kuiandika katika mioyo yao. Mimi nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

34. Wala haitawabidi kufundishana na kusema: ‘Mjue Mwenyezi-Mungu’, kwa sababu wote, wadogo kwa wakubwa, watanijua mimi Mungu. Maana nitawasamehe makosa yao, wala sitazikumbuka tena dhambi zao.”

35. Hivi ndivyo asemavyo Mwenyezi-Mungu, ambaye jina lake ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi, aliyepanga jua liangaze mchana, mwezi na nyota vimulike usiku, na aifanyaye bahari iwe na mawimbi:

36. Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Mimi hulifanya jua liangaze mchana, mwezi na nyota vimulike usiku; pia mimi huitikisa bahari, nayo hutoa mawimbi. Jina langu mimi ni Mwenyezi-Mungu wa majeshi. Basi, nami nasema: Kadiri ninavyotegemeza mipango hiyo yote yangu kadiri hiyohiyo Israeli watakavyobaki kuwa watu wangu.

37. Kama mbingu zaweza kupimwa, na misingi ya dunia kuchunguzwa, basi, nitawatupilia mbali wazawa wa Israeli, kwa sababu ya mambo yote waliyotenda. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

38. Mwenyezi-Mungu asema: “Siku zaja ambapo mji huu wa Yerusalemu utajengwa upya kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu, kutoka mnara wa Hananeli hadi Lango la Pembeni.

39. Nayo kamba ya kupimia itanyoshwa moja kwa moja hadi mlima Garebu, kisha itazungushwa hadi Goa.

40. Bonde lote walimozikwa wafu na kutupiwa majivu, mashamba yote, mpaka kijito cha Kidroni, mpaka pembe ya lango la Farasi kuelekea mashariki, litakuwa eneo takatifu kwa Mwenyezi-Mungu. Hakuna kitakachoharibiwa humo wala kubomolewa tena milele.”

Kusoma sura kamili Yeremia 31