Agano la Kale

Agano Jipya

Yeremia 13:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu aliniambia hivi: “Nenda ukajinunulie kikoi cha kitani, ukajifunge kiunoni; lakini usikitie majini.”

2. Basi, nikaenda, nikanunua kikoi kama alivyoniagiza Mwenyezi-Mungu, nikajifunga kiunoni.

3. Kisha, neno la Mwenyezi-Mungu likanijia mara ya pili:

4. “Kichukue kikoi ulichonunua na ambacho umejifunga kiunoni, uende kwenye mto Eufrate na kukificha katika pango mwambani.”

5. Basi, nikaenda na kukificha kikoi hicho karibu na mto Eufrate, kama Mwenyezi-Mungu alivyoniamuru.

6. Ikawa, baada ya siku nyingi, Mwenyezi-Mungu akaniambia, “Nenda kwenye mto Eufrate, ukakichukue kile kikoi nilichokuamuru ukifiche huko.”

7. Basi, nikaenda kwenye mto Eufrate, nikachimbua na kukitoa kile kikoi mahali nilipokuwa nimekificha. Nilipokitoa, nilishangaa kukiona kuwa kilikuwa kimeharibika kabisa; kilikuwa hakifai tena.

8. Ndipo neno la Mwenyezi-Mungu likanijia:

9. “Mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Hivi ndivyo nitakavyokiharibu kiburi cha Yuda na kiburi kikubwa cha Yerusalemu.

10. Watu hawa waovu wanakataa kusikia maneno yangu, na badala yake wanakuwa wakaidi na kufuata mawazo yao wenyewe. Wanaifuata miungu mingine, wanaitumikia na kuiabudu. Hao watakuwa kama kikoi hiki ambacho hakifai kitu.

11. Kama vile kikoi kinavyoshikamana na kiuno cha mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami watu wa Israeli na watu wa Yuda, ili wajulikane kwa jina langu, wanisifu na kunitukuza. Lakini wao hawakunisikiliza. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”

12. Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, aliniambia hivi: “Waambie watu wa Israeli kwamba kila mtungi utajazwa divai. Lakini utakapowaambia hivyo, wao watakujibu hivi: ‘Kwani unadhani sisi hatujui kwamba kila mtungi utajazwa divai?’

13. Nawe utawaambia kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Nitawalewesha wenyeji wote wa nchi hii; wafalme wanaotawala mahali pa Daudi, makuhani, manabii na wakazi wote wa Yerusalemu.

Kusoma sura kamili Yeremia 13