Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 26:31-44 Biblia Habari Njema (BHN)

31. Miji yenu nitaiteketeza mahali penu patakatifu nitapafanya jangwa na harufu zenu nzuri za sadaka kamwe sitazikubali.

32. Nitaiteketeza nchi yenu hivyo kwamba hata adui wanaohamia humo watashangaa.

33. Nitawatawanya nyinyi miongoni mwa watu wa mataifa na kuchomoa upanga dhidi yenu. Nchi yenu itakuwa ni ukiwa na miji yenu uharibifu.

34. “Nyinyi mtakapokuwa mikononi mwa adui zenu, hapo ndipo nchi itakapozifurahia sabato zake wakati itakapokuwa hali ya ukiwa. Nchi itapumzika na kufurahia sabato zake.

35. Kadiri itakapokuwa hali ya ukiwa itapata kiasi ambacho haikupata katika sabato zenu mlipokuwa mkiishi humo.

36. Na kwa baadhi yenu watakaosalimika nitawaletea woga mioyoni mwao, katika nchi ya adui zao hata jani linalopeperushwa litawakimbiza. Watakimbia kama mtu anayekimbia vita. Watakimbia na kuanguka hata kama hamna mtu anayewafukuza.

37. Wataangukiana ovyo kama mtu anayekimbia vita hata kama hamna anayewafukuza. Hamtakuwa na nguvu yoyote kuwakabili adui zenu.

38. Mtaangamia kati ya mataifa na nchi za adui zenu zitawameza.

39. Kama baadhi yenu wakisalimika katika nchi za adui zenu watadhoofika kwa sababu ya uovu wao; na kwa sababu ya uovu wa wazee wao.

40. “Lakini kama wakitubu uovu wao na uovu wa wazee wao juu ya uasi waliotenda dhidi yangu na pia juu ya kupingana kwao nami,

41. wakatambua kwa nini nilipingana nao na kuwapeleka katika nchi ya adui zao; kama kweli moyo wao mkaidi ukinyenyekea na kutubu uovu wao,

42. basi, hapo nami nitalikumbuka agano langu na Abrahamu, Isaka na Yakobo; na kuikumbuka ile nchi niliyowaahidia.

43. “Wakati watakapokuwa nje ya nchi yao, nchi hiyo itafurahia sabato zake hapo itakapokuwa hali ya ukiwa. Wakati huo wao watatubu uovu wao wa kupuuza maagizo yangu na kuyachukia maagizo yangu.

44. Lakini, kwa hayo yote, wawapo katika nchi ya adui zao; mimi sitawatupa wala kuwachukia hata kuwaangamiza kabisa na kulivunjilia mbali agano langu.

Kusoma sura kamili Walawi 26