Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
  17. 17
  18. 18
  19. 19
  20. 20
  21. 21
  22. 22
  23. 23
  24. 24
  25. 25
  26. 26
  27. 27

Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 26 Biblia Habari Njema (BHN)

Baraka kwa utiifu

1. “Msijitengenezee sanamu za miungu ya uongo, msishike sanamu zao za kuchonga wala nguzo wala sanamu za mawe yaliyochongwa nchini mwenu na kuvisujudu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.

2. Shikeni sabato zangu na kuheshimu mahali pangu patakatifu. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.

3. “Kama mkifuata masharti yangu na kuzishika amri zangu,

4. nitawanyeshea mvua wakati ufaao, nchi ipate kuzaa mavuno kwa wingi, nayo miti ya mashambani matunda yake.

5. Kupura nafaka kutaendelea mpaka wakati wa kuvuna zabibu, na uvunaji zabibu mpaka wakati wa kupanda mbegu. Mtakuwa na chakula tele na kuishi kwa usalama nchini mwenu.

6. Nitawapeni amani nchini hata muweze kulala bila ya kuogopeshwa na chochote. Nitawaondoa wanyama wakali katika nchi na nchi yenu haitakumbwa na vita.

7. Mtawafukuza adui zenu na kuwaua kwa upanga.

8. Watano wenu watawafukuza adui 100 na 100 wenu watawafukuza adui 10,000. Adui zenu wataangamia mbele yenu kwa upanga.

9. Nitawafadhili na kuwajalia mpate watoto wengi na kuongezeka; nami nitaliimarisha agano langu nanyi.

10. Wakati wa mavuno mtakuwa bado mnakula mazao ya zamani; tena itawalazimu kuondoa yaliyobaki kupata nafasi ya kuhifadhi mavuno mapya.

11. Nitaweka maskani yangu miongoni mwenu, wala sitawaacheni.

12. Nitatembea kati yenu na kuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu.

13. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, niliyewatoa nchini Misri ili msiwe watumwa wa Wamisri. Mimi nimevunja nira mliyofungiwa shingoni mwenu na kuwafanya mtembee wima.

Laana

14. “Lakini kama hamtanisikiliza wala kufuata amri zangu,

15. kama mkidharau masharti yangu na kuchukia kwa roho maagizo yangu mkaacha kuzitii amri zangu zote na kuvunja agano langu,

16. basi, mimi nitafanya hivi: Nitawapiga kwa kuwaletea hofu kuu ya ghafla, kifua kikuu na homa itakayowapofusha macho na kuwadhoofisha. Mtapanda mbegu zenu bila mafanikio kwani adui zenu ndio watakaokula.

17. Mimi nitawakabili, nanyi mtapigwa na adui zenu; mtatawaliwa na wale wanaowachukia. Mtatishwa na kukimbia hata kama hakuna mtu yeyote anayewafukuza.

18. Na Kama hata baada ya kuadhibiwa hivyo, hamtanisikiliza, basi, nitawaadhibu mara saba zaidi kwa ajili ya dhambi zenu.

19. Kiburi chenu nitakivunjilia mbali kwa kuzifanya mbingu huko juu kuwa ngumu kama chuma, na nchi yenu bila mvua iwe ngumu kama shaba.

20. Mtatumia nguvu zenu bure maana mashamba yenu hayatatoa mavuno na nchi yenu haitazaa matunda.

21. “Kama mkiendelea kunipinga na kukataa kunisikiliza, nitazidisha tena adhabu yenu mara saba kadiri ya wingi wa dhambi zenu.

22. Nitawapeleka wanyama wakali kati yenu ambao watawanyakulieni watoto wenu na kula mifugo yenu; na kukata idadi yenu hata njia zenu zigeuke kama jangwa.

23. “Kama hata baada ya adhabu hiyo bado hamnigeukii mimi, ila mnazidi kupingana nami,

24. basi, nami nitapingana nanyi na kuwaadhibu mara saba zaidi kwa ajili ya dhambi zenu.

25. Nitawaleteeni upanga ambao utalipiza kisasi juu ya agano mlilovunja. Nyinyi mtakimbilia katika miji yenu, lakini nitawapelekea maradhi mabaya na kuwatia mikononi mwa adui zenu.

26. Chakula chenu nitakipunguza hata wanawake kumi watumie jiko moja tu kuoka mikate. Watawagawia kwa kipimo. Na hata baada ya kula bado mtakuwa na njaa tu.

27. “Na kama hata baada ya hayo yote bado hamtanisikiliza mkaendelea kunipinga,

28. basi nami nitapingana nanyi kwa hasira kali, na kuwaadhibu mimi mwenyewe mara saba zaidi kwa ajili ya dhambi zenu.

29. Ndipo mtakula watoto wenu, wa kiume na kike.

30. Nitapaharibu mahali penu pa ibada milimani, nitazibomoa madhabahu zenu za kufukizia ubani, na kuzitupa maiti zenu juu ya sanamu za miungu yenu. Roho yangu itawachukia kabisa.

31. Miji yenu nitaiteketeza mahali penu patakatifu nitapafanya jangwa na harufu zenu nzuri za sadaka kamwe sitazikubali.

32. Nitaiteketeza nchi yenu hivyo kwamba hata adui wanaohamia humo watashangaa.

33. Nitawatawanya nyinyi miongoni mwa watu wa mataifa na kuchomoa upanga dhidi yenu. Nchi yenu itakuwa ni ukiwa na miji yenu uharibifu.

34. “Nyinyi mtakapokuwa mikononi mwa adui zenu, hapo ndipo nchi itakapozifurahia sabato zake wakati itakapokuwa hali ya ukiwa. Nchi itapumzika na kufurahia sabato zake.

35. Kadiri itakapokuwa hali ya ukiwa itapata kiasi ambacho haikupata katika sabato zenu mlipokuwa mkiishi humo.

36. Na kwa baadhi yenu watakaosalimika nitawaletea woga mioyoni mwao, katika nchi ya adui zao hata jani linalopeperushwa litawakimbiza. Watakimbia kama mtu anayekimbia vita. Watakimbia na kuanguka hata kama hamna mtu anayewafukuza.

37. Wataangukiana ovyo kama mtu anayekimbia vita hata kama hamna anayewafukuza. Hamtakuwa na nguvu yoyote kuwakabili adui zenu.

38. Mtaangamia kati ya mataifa na nchi za adui zenu zitawameza.

39. Kama baadhi yenu wakisalimika katika nchi za adui zenu watadhoofika kwa sababu ya uovu wao; na kwa sababu ya uovu wa wazee wao.

40. “Lakini kama wakitubu uovu wao na uovu wa wazee wao juu ya uasi waliotenda dhidi yangu na pia juu ya kupingana kwao nami,

41. wakatambua kwa nini nilipingana nao na kuwapeleka katika nchi ya adui zao; kama kweli moyo wao mkaidi ukinyenyekea na kutubu uovu wao,

42. basi, hapo nami nitalikumbuka agano langu na Abrahamu, Isaka na Yakobo; na kuikumbuka ile nchi niliyowaahidia.

43. “Wakati watakapokuwa nje ya nchi yao, nchi hiyo itafurahia sabato zake hapo itakapokuwa hali ya ukiwa. Wakati huo wao watatubu uovu wao wa kupuuza maagizo yangu na kuyachukia maagizo yangu.

44. Lakini, kwa hayo yote, wawapo katika nchi ya adui zao; mimi sitawatupa wala kuwachukia hata kuwaangamiza kabisa na kulivunjilia mbali agano langu.

45. La! Kwa ajili yao nitalikumbuka agano nililofanya na wazee wao ambao niliwatoa katika nchi ya Misri, mataifa yakishuhudia, ili mimi niwe Mungu wao. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.”

46. Hayo ndiyo masharti, maagizo na sheria ambazo Mwenyezi-Mungu aliwapa watu wa Israeli kule mlimani Sinai kwa njia ya Mose.