Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 15:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose na Aroni,

2. “Waambieni Waisraeli hivi: Mwanamume yeyote akitokwa na usaha, usaha huo wamfanya kuwa najisi.

3. Na ufuatao ni mwongozo kuhusu najisi hiyo: Muda wote anapotokwa na usaha au usaha unapokuwa umezuiwa ndani yake, mtu huyo ni najisi.

4. Kitanda chochote atakacholalia au atakachokalia, kitakuwa najisi.

5. Mtu yeyote atakayegusa kitanda chake mtu huyo ni lazima ayafue mavazi yake, na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni.

6. Mtu yeyote atakayekalia kitu chochote alichokalia huyo mtu mwenye kutokwa na usaha, ni lazima ayafue mavazi na kuoga; na atakuwa najisi hadi jioni.

7. Mtu yeyote atakayemgusa mtu atokwaye na usaha, lazima afue mavazi yake na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni.

8. Mtu yeyote akitemewa mate na mtu anayetokwa usaha ni lazima mtu huyo aliyetemewa mate ayafue mavazi yake, na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni.

9. Tandiko lolote la mnyama aliloketia mtu anayetokwa na usaha litakuwa najisi.

10. Mtu yeyote atakayegusa kitu chochote alichokalia mtu huyo, atakuwa najisi mpaka jioni. Mtu yeyote anayebeba kitu chochote kilichokuwa cha mtu huyo ni lazima ayafue mavazi yake, na kuoga; naye atakuwa najisi mpaka jioni.

11. Mtu yeyote anayetokwa na usaha akimgusa mtu bila kusafisha kwanza mikono yake na kuoga, aliyeguswa atakuwa najisi mpaka jioni.

12. Chombo chochote cha udongo kilichoguswa na mtu anayetokwa na usaha ni lazima kivunjwe. Lakini chombo chochote cha mbao ni lazima kisafishwe kwa maji.

13. “Mwanamume yeyote anayetokwa na usaha akiponywa ugonjwa wake, ni lazima huyo mtu angoje siku saba kabla ya kuondolewa unajisi wake. Atayafua mavazi yake na kuoga kwa maji ya mtoni; naye atakuwa safi.

14. Siku ya nane, ni lazima alete hua wawili au makinda mawili ya njiwa mbele ya Mwenyezi-Mungu mlangoni mwa hema la mkutano na kumkabidhi kuhani.

15. Kuhani atawatoa hao, mmoja kwa ajili ya sadaka ya kuondoa dhambi na mwingine kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atamfanyia huyo mtu ibada ya upatanisho mbele ya Mwenyezi-Mungu na kumwondolea unajisi wake wa kutokwa na usaha.

Kusoma sura kamili Walawi 15