Agano la Kale

Agano Jipya

Walawi 13:27-39 Biblia Habari Njema (BHN)

27. Siku ya saba kuhani atamwangalia. Kama umeenea kwenye ngozi, basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; kwani anao ugonjwa wa ukoma.

28. Lakini, kama ile alama haijaenea, ila imefifia, huo ni uvimbe uliotokana na kuungua; basi, kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi; kwani hilo ni kovu la kuungua.

29. “Kama mtu yeyote mwanamume au mwanamke, ana kidonda kichwani au kidevuni,

30. kuhani atauangalia ugonjwa huo. Iwapo kuhani ataona kuwa kuna shimo na nywele ni manjano na nyembamba, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa najisi; kwani huo ni upele na ni ukoma wa kichwa au wa kidevu.

31. Kama kuhani ataona kuwa hakuna shimo na nywele si nyeusi, basi kuhani atamtenga mtu huyo kwa muda wa siku saba.

32. Siku ya saba kuhani atakiangalia kile kidonda. Kama kidonda hicho hakijaenea na hakuna nywele zenye rangi ya manjano wala hakuna vipele vyovyote mahali hapo, basi,

33. mtu huyo atanyoa nywele au ndevu zake. Lakini mahali pale penye vipele hatapanyoa. Kisha kuhani atamtenga mtu huyo kwa muda mwingine wa siku saba.

34. Siku ya saba, kuhani ataviangalia vile vipele. Iwapo kuhani ataona kuwa vipele hivyo havikuenea kwenye ngozi na wala havikwenda ndani ya ngozi, basi, atamtangaza mtu huyo kuwa safi. Mtu huyo atafua mavazi yake, naye atakuwa safi.

35. Lakini iwapo vipele hivyo vimeenea baada ya kutakaswa,

36. mtu huyo ataangaliwa na kuhani na ikiwa vimeenea kwenye ngozi, kuhani hatahitaji kutafuta nywele zenye rangi manjano; mtu huyo atakuwa najisi.

37. Lakini iwapo kuhani ataona kuwa vile vipele vimepona na nywele nyeusi zimeota mahali hapo, basi, vidonda hivyo vimepona, basi, mtu huyo ni safi. Kuhani atamtangaza mtu huyo kuwa safi.

38. “Kama mtu yeyote, awe mwanamume au mwanamke, ana alama nyeupe mwilini mwake,

39. kuhani atamwangalia mtu huyo. Iwapo kuhani ataona kuwa alama hizo ni nyeupe kiasi, huo ni upele wa kawaida; mtu huyo ni safi.

Kusoma sura kamili Walawi 13