Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 8:21-31 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Hapo Zeba na Salmuna wakasema, “Tuue wewe mwenyewe, maana hii ni kazi ya mtu mzima.” Gideoni akawaua yeye mwenyewe na kuchukua mapambo yao yaliyokuwa shingoni mwa ngamia wao.

22. Kisha, Waisraeli wakamwambia Gideoni, “Wewe na uwe mtawala wetu, na baada yako watutawale wazawa wako, kwa kuwa wewe umetukomboa kutoka kwa Wamidiani.”

23. Gideoni akawajibu, “Mimi sitakuwa mtawala wenu wala mwanangu hatakuwa mtawala wenu. Mwenyezi-Mungu ndiye atakayekuwa mtawala wenu.”

24. Kisha akawaambia, “Ningependa kuwaomba kitu kimoja; naomba kila mmoja wenu anipe vipuli mlivyoteka nyara.” Wale Wamidiani kwa vile walikuwa Waishmaeli, walivaa vipuli vya dhahabu.

25. Watu wakamjibu, “Tutakupa kwa hiari.” Wakatandaza nguo na kila mmoja akatupa humo vipuli walivyokuwa wameteka nyara.

26. Uzito wa vipuli vyote alivyowataka wampe ulikuwa kilo ishirini. Zaidi ya hivyo, alipokea pia herini, mavazi ya urujuani yaliyovaliwa na wafalme wa Midiani na mikufu iliyokuwa kwenye shingo za ngamia wao.

27. Gideoni akazitumia kutengenezea kizibao ambacho alikiweka kwenye mji wake wa Ofra. Waisraeli wote wakaenda huko kukiabudu. Kizibao hicho kikawa mtego kwa Gideoni na jamaa yake.

28. Basi, Wamidiani walishindwa kabisa wasiwe tishio kwa Israeli; na nchi ya Israeli ikawa na amani kwa muda wa miaka arubaini.

29. Gideoni, yaani Yerubaali, mwana wa Yoashi akarudi nyumbani kwake na kukaa huko.

30. Gideoni alikuwa na watoto wa kiume sabini, maana alioa wanawake wengi.

31. Alikuwa na suria huko Shekemu ambaye alimzalia mtoto wa kiume, jina lake Abimeleki.

Kusoma sura kamili Waamuzi 8