Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 7:5-17 Biblia Habari Njema (BHN)

5. Basi, Gideoni akawapeleka watu mtoni na Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Watu watakaoramba maji kama mbwa, utawatenganisha na wale watakaopiga magoti kunywa maji.”

6. Idadi ya waliokunywa maji kwa kuchota kwa mikono yao na kuramba kama mbwa ilikuwa 300. Lakini wengine wote waliobaki walipiga magoti kunywa maji.

7. Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Kwa hao watu 300 waliokunywa kwa kuramba kama mbwa, nitawaokoa Waisraeli na kuwatia Wamidiani mikononi mwao. Lakini wale wengine wote warudi makwao.”

8. Basi, Gideoni akachukua vyakula vya wale waliokuwa wanaondoka na tarumbeta, akawaaga waende makwao. Yeye akabaki na wale watu 300. Kambi ya Wamidiani ilikuwa bondeni upande wao wa chini.

9. Usiku huo, Mwenyezi-Mungu akamwambia Gideoni, “Nenda ukawashambulie kambini mwao, maana nimewatia mikononi mwako.

10. Lakini kama unaogopa, nenda pamoja na mtumishi wako Pura.

11. Huko utasikia wanayosema, nawe utapata nguvu za kuweza kwenda kuwashambulia.” Basi, Gideoni akaenda pamoja na mtumishi wake Pura mpaka kwenye vituo vya walinda zamu wa kambi ya Wamidiani.

12. Wamidiani, Waamaleki na watu wote wa Mashariki walilala bondeni, wengi kama nzige, na ngamia wao wasiohesabika, wengi kama mchanga wa pwani.

13. Gideoni alipofika, akamsikia mtu mmoja akimsimulia mwenzake ndoto yake hivi: “Niliota ndoto. Niliona mkate wa shayiri ukivingirika hadi kambini mwa Wamidiani, ukalipiga hema na kulipindua chini juu. Hema likalala chini.”

14. Mwenzake akamjibu, “Hiyo inamaanisha tu upanga wa yule Mwisraeli Gideoni mwana wa Yoashi ambaye mikononi mwake Mungu amewatia Wamidiani pamoja na jeshi lote.”

15. Gideoni aliposikia masimulizi hayo ya ndoto na tafsiri yake, alimwabudu Mungu. Kisha alirudi kwenye kambi ya Waisraeli, akasema, “Amkeni twende; maana Mwenyezi-Mungu amelitia jeshi la Wamidiani mikononi mwenu.”

16. Basi akawagawa wale watu 300 katika makundi matatu, akawapa tarumbeta na magudulia yenye mienge.

17. Akawaambia, “Mniangalie na kufanya sawa kama nitakavyofanya wakati nitakapofika kambini.

Kusoma sura kamili Waamuzi 7