Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 4:14-24 Biblia Habari Njema (BHN)

14. Debora akamwambia Baraki, “Inuka! Leo ni siku ambayo Mwenyezi-Mungu atamtia Sisera mikononi mwako. Mwenyezi-Mungu anakwenda mbele yako.” Basi, Baraki akashuka kutoka mlimani Tabori akiwaongoza watu wake 10,000.

15. Baraki akafanya mashambulizi, naye Mwenyezi-Mungu akamtimua Sisera na jeshi lake lote mbele ya Baraki kwa upanga. Sisera akatoka katika gari lake, akakimbia kwa miguu.

16. Baraki akalifuatia jeshi hilo na magari mpaka Harosheth-hagoimu na kuwaua wanajeshi wote wa Sisera kwa mapanga; hakubaki hata mtu mmoja.

17. Lakini Sisera alikimbia kwa miguu mpaka hemani kwa Yaeli, mke wa Heberi, Mkeni. Alifanya hivyo kwa sababu kulikuwa na amani kati ya mfalme Yabini wa Hazori na jamaa ya Heberi.

18. Yaeli akatoka kumlaki Sisera, akamwambia, “Bwana wangu, karibu kwangu, wala usiogope.” Akaingia hemani mwake, akamfunika kwa blanketi.

19. Sisera akamwambia Yaeli, “Tafadhali, nipe maji kidogo ninywe, maana nina kiu.” Akampa maziwa badala ya maji, kisha akamfunika tena.

20. Sisera akamwambia, “Simama mlangoni mwa hema. Mtu yeyote akija kukuuliza kama kuna mtu yeyote hapa, mwambie hakuna.”

21. Lakini Yaeli, mke wa Heberi, akachukua kigingi cha hema na nyundo, akamwendea polepole akakipigilia kile kigingi cha hema katika paji la uso wake kikapenya mpaka udongoni, kwa maana alikuwa amelala fofofo kwa uchovu. Basi, Sisera akafa papo hapo.

22. Naye Baraki alipokuwa anamfuatilia Sisera, Yaeli akatoka nje kumlaki akamwambia, “Njoo nami nitakuonesha yule unayemtafuta.” Baraki akaingia ndani ya hema la Yaeli na kumkuta Sisera chini, amekufa, na kigingi cha hema pajini mwake.

23. Hivyo, siku hiyo Mungu akawapa Waisraeli ushindi juu ya mfalme Yabini wa Kanaani.

24. Waisraeli wakaendelea kumwandama Yabini, mfalme wa Kanaani, mpaka walipomwangamiza.

Kusoma sura kamili Waamuzi 4