Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 19:15-22 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Wakaingia mjini wapate kulala humo usiku. Walipoingia mjini wakaenda kukaa kwenye uwanja wa wazi wa mji, kwani hakuna mtu aliyewakaribisha nyumbani kwake.

16. Walipokuwa huko mzee mmoja akafika kutoka shambani kwake. Mzee huyo alikuwa mwenyeji wa nchi ya milima ya Efraimu na alikuwa akiishi huko Gibea kama mgeni. Wakazi wa mji wa Gibea walikuwa wa kabila la Benyamini.

17. Mzee huyo alipotazama na kumwona huyo msafiri akiwa huko uwanjani, alimwuliza, “Umetoka wapi na unakwenda wapi?”

18. Naye akamjibu, “Tumetoka Bethlehemu nchini Yuda na tunaelekea sehemu za mbali za eneo la milima ya Efraimu. Huko ndiko ninakoishi na sasa ninarudi safarini huko Bethlehemu katika Yuda na kurejea nyumbani; hakuna mtu hapa aliyetukaribisha nyumbani kwake.

19. Lakini sisi watumishi wako tuna nyasi na malisho kwa ajili ya punda wetu. Pia nina mkate na divai; hivyo vinanitosha mimi, suria wangu na mtumishi wangu. Hatupungukiwi kitu chochote.”

20. Huyo mzee akamwambia, “Amani iwe nanyi! Nitawapa mahitaji yote. Ila msilale huku uwanjani.”

21. Hivyo akawapeleka nyumbani kwake na kuwapa punda wao malisho. Hao wasafiri wakanawa miguu yao, wakala na kunywa.

22. Walipokuwa wanajifurahisha, kumbe wanaume mabaradhuli wa mji huo wakaja wakaizingira hiyo nyumba na kugonga mlangoni. Wakamwambia mzee mwenye nyumba, “Mtoe nje yule mwanamume aliyekuja kwako, tulale naye.”

Kusoma sura kamili Waamuzi 19