Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 19:11-19 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Walipokuwa wamekaribia mjini Yebusi, siku ilikuwa karibu imekwisha; naye mtumishi akamwambia bwana wake, “Sasa heri tuingie katika mji huu wa Wayebusi tulale humo usiku huu.”

12. Bwana wake akamjibu, “Hatutageuka na kuingia katika mji wa wageni ambao si Waisraeli. Tutaendelea na safari mpaka Gibea.

13. Twende tukaribie sehemu hizo na kulala huko Gibea au Rama.”

14. Basi, wakaendelea na safari yao mpaka jua likatua wakiwa karibu na mji wa Gibea ambao ni mji wa kabila la Benyamini.

15. Wakaingia mjini wapate kulala humo usiku. Walipoingia mjini wakaenda kukaa kwenye uwanja wa wazi wa mji, kwani hakuna mtu aliyewakaribisha nyumbani kwake.

16. Walipokuwa huko mzee mmoja akafika kutoka shambani kwake. Mzee huyo alikuwa mwenyeji wa nchi ya milima ya Efraimu na alikuwa akiishi huko Gibea kama mgeni. Wakazi wa mji wa Gibea walikuwa wa kabila la Benyamini.

17. Mzee huyo alipotazama na kumwona huyo msafiri akiwa huko uwanjani, alimwuliza, “Umetoka wapi na unakwenda wapi?”

18. Naye akamjibu, “Tumetoka Bethlehemu nchini Yuda na tunaelekea sehemu za mbali za eneo la milima ya Efraimu. Huko ndiko ninakoishi na sasa ninarudi safarini huko Bethlehemu katika Yuda na kurejea nyumbani; hakuna mtu hapa aliyetukaribisha nyumbani kwake.

19. Lakini sisi watumishi wako tuna nyasi na malisho kwa ajili ya punda wetu. Pia nina mkate na divai; hivyo vinanitosha mimi, suria wangu na mtumishi wangu. Hatupungukiwi kitu chochote.”

Kusoma sura kamili Waamuzi 19