Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 18:21-29 Biblia Habari Njema (BHN)

21. Basi, wakaanza safari yao, huku wametanguliwa na watoto wao na mifugo na mali zao.

22. Walipokuwa wamefika mbali na nyumbani kwa Mika, watu waliokuwa jirani na Mika wakaitwa, wakawafuatia watu wa kabila la Dani wakawafikia.

23. Kisha wakawapigia kelele, nao watu wa kabila la Dani wakageuka, wakamwuliza Mika, “Una shida gani hata umetufuatia pamoja na kundi hili lote?”

24. Mika akasema, “Nyinyi mmechukua miungu yangu niliyojitengenezea, mkamchukua na kuhani wangu, mkaniacha bila chochote. Mnawezaje basi kuniuliza nina shida gani?”

25. Watu wa kabila la Dani wakamwambia, “Afadhali uache kelele zako, la sivyo wengine wetu wenye hasira wanaweza wakakuvamia, nawe ukapoteza maisha yako na maisha ya jamaa yako.”

26. Mika alipoona kwamba wamemzidi nguvu, akageuka, akarudi nyumbani; nao watu wa kabila la Dani wakaenda zao.

27. Hao watu wa kabila la Dani walivichukua vitu vile ambavyo Mika alikuwa amevitengeneza, wakamchukua na yule kuhani aliyemhudumia. Basi wakaenda kushambulia Laishi wakawaua wakazi wake ambao waliishi humo kwa utulivu na bila wasiwasi, wakauteketeza mji huo.

28. Wakazi wa mji huo hawakuwa na mtu wa kuwaokoa kwa sababu walikuwa mbali na mji wa Sidoni, tena hawakuwa na uhusiano na watu wengine. Mji huo ulikuwa kwenye bonde la Beth-rehobu. Watu wa kabila la Dani wakaujenga upya, wakaishi humo.

29. Walibadilisha jina la mji huo, wakauita Dani, kufuata jina la babu yao aliyekuwa mwana wa Israeli. Lakini mji huo hapo awali uliitwa Laishi.

Kusoma sura kamili Waamuzi 18