Agano la Kale

Agano Jipya

Waamuzi 11:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Huko Gileadi kulikuwa na mpiganaji hodari aitwaye Yeftha, mwana wa mama mmoja malaya, na baba yake aliitwa Gileadi.

2. Gileadi alikuwa pia na wana wengine kwa mke wake wa halali. Watoto wa mke huyo walipokuwa wakubwa, walimfukuza Yeftha kutoka nyumbani, wakamwambia, “Wewe huna haki ya kupata urithi kutoka kwa baba yetu, maana wewe ni mtoto wa mwanamke mwingine.”

3. Basi, Yeftha akawakimbia ndugu zake akaenda kuishi katika nchi ya Tobu. Huko watu ovyo wakakusanyika kujiunga naye, wakamfuata katika safari zake za mashambulio.

4. Baada ya muda fulani, Waamoni waliwashambulia Waisraeli.

5. Wakati vita vilipopamba moto, wazee wa Gileadi wakaenda kumleta Yeftha kutoka nchi ya Tobu,

6. wakamwambia, “Njoo utuongoze katika vita vyetu na Waamoni.”

7. Lakini Yeftha akawaambia hao wazee wa Gileadi, “Je, si mlinichukia hata mkanifukuza kutoka kwa jamaa ya baba yangu? Kwa nini mnanijia sasa mkiwa katika taabu?”

8. Hao wazee wa Gileadi wakamwambia “Ndio maana tumekujia ili uende nasi kupigana na Waamoni, nawe utakuwa kiongozi wetu na wa wakazi wote wa Gileadi.”

9. Yeftha akawaambia hao wazee wa Gileadi, “Kama mkinirudisha nyumbani kupigana na Waamoni halafu Mwenyezi-Mungu akawatia mikononi mwangu, mimi nitakuwa kiongozi wenu.”

10. Wale wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, “Mwenyezi-Mungu atakuwa shahidi kati yetu. Hakika tutafanya kama ulivyosema.”

11. Yeftha akafuatana na wazee wa Gileadi, nao watu wakamfanya kiongozi wao. Yeftha akasema masharti yake huko Mizpa mbele ya Mwenyezi-Mungu

12. Yeftha akapeleka ujumbe kwa mfalme wa Amoni akamwambia, “Una ugomvi gani nasi hata uje kuishambulia nchi yetu?”

Kusoma sura kamili Waamuzi 11