Agano la Kale

Agano Jipya

Nehemia 8:1-7 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Kisha watu wote, kwa nia moja, wakakusanyika mjini Yerusalemu kwenye uwanja ulio karibu na Lango la Maji. Wakamwambia Ezra, mwandishi, kukileta kitabu cha sheria ya Mose ambayo Mwenyezi-Mungu aliwapa watu wa Israeli.

2. Ezra, ambaye alikuwa kuhani, akaenda na kukileta kitabu cha sheria ya Mose mbele ya mkutano mzima, wanaume kwa wanawake na yeyote aliyeweza kuielewa hiyo sheria aliposikia. Siku hiyo ilikuwa ni siku ya kwanza ya mwezi wa saba.

3. Kisha watu wote wanaume kwa wanawake na yeyote aliyeweza kuelewa, Ezra aliwasomea sheria ya Mose akiwa mbele ya Lango la Maji tangu asubuhi hadi adhuhuri. Watu wote wakatega masikio yao kusikiliza kwa makini kitabu cha sheria.

4. Ezra, mwandishi, alikuwa amesimama kwenye mimbari ya mbao iliyotengenezwa kwa kusudi hilo; na kwenye mkono wake wa kulia walikuwa wamesimama Matithia, Shema, Anaya, Uria, Hilkia na Maaseya; na kwenye mkono wake wa kushoto walikuwa wamesimama Pedaya, Mishaeli, Malkiya, Hashumu, Hashbadana, Zekaria na Meshulamu.

5. Ezra akasimama kwenye mimbari, mbele ya watu wote, nao wakawa wanamkazia macho yao kwa utulivu mkubwa. Mara tu Ezra alipokifungua kitabu cha sheria, watu wote wakasimama wima.

6. Ezra akamshukuru Mwenyezi-Mungu, Mungu Mkuu na watu wote wakaitikia “Amina! Amina!” Huku wakiwa wameinua mikono yao juu. Kisha wakamsujudia Mungu huku nyuso zao zikigusa ardhi.

7. Walawi wafuatao walisaidia kuwaelewesha watu sheria: Yeshua, Bani, Sherebia, Yamini, Akubu, Shabethai, Hodia, Maaseya, Kelita, Azaria, Yozabadi, Hanani na Pelaya; walifanya hivyo kila mmoja akiwa amesimama mahali pake.

Kusoma sura kamili Nehemia 8