Agano la Kale

Agano Jipya

Nehemia 4:8-17 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Wakala njama kwa pamoja kuja Yerusalemu kutushambulia na hivyo kuleta mvurugano katika mji huo.

9. Ndipo tulipomwomba Mungu wetu na kuweka ulinzi dhidi yao, mchana na usiku.

10. Watu wa Yuda wakawa wakilalamika wakisema, “Nguvu za vibarua zinapungua na bado kuna takataka nyingi za kubeba. Hatuwezi kuendelea kujenga ukuta.”

11. Nao adui zetu wakawa wanasema, “Hawataweza kujua wala kuona, hadi tutakapofika kwao na kuwaua na kusimamisha kazi.”

12. Wayahudi waliokaa miongoni mwa adui zetu waliposikia maneno yao, walitujia mara kumi wakisema, “Watakuja toka kila mahali wanapokaa na kutushambulia.”

13. Hivyo, kwenye sehemu za chini za ukuta ambazo zilikuwa bado kumalizika, nyuma ya ukuta, katika mahali pa wazi, niliwapanga watu kulingana na jamaa zao wakiwa na mapanga, mikuki na pinde.

14. Nilipoona kuwa watu walikuwa na hofu nikawaambia wakuu, maofisa na watu wote kwa ujumla, “Msiwaogope hata kidogo. Mkumbukeni Bwana aliye Mkuu na wa kutisha, basi piganeni kwa ajili ya ndugu zenu, wana wenu, binti zenu, wake zenu na nyumba zenu.”

15. Maadui waliposikia kwamba njama zao tumezigundua na kuwa Mungu amevuruga njama hizo, ndipo sisi sote tulipourudia ukuta, kila mmoja akaendelea na kazi yake.

16. Tokea siku hiyo na kuendelea, nusu ya watumishi wangu wakawa wanaendelea na ujenzi ambapo nusu nyingine ikawa inashika ulinzi wakiwa na mikuki, ngao, pinde na mavazi ya kukinga kifua. Viongozi wetu wakawa upande wa watu wa Yuda

17. waliokuwa wanaujenga ukuta. Hata wale waliokuwa wanabeba vifaa vya ujenzi waliendelea na kazi huku mkono mmoja ukiwa na vifaa vya ujenzi na mkono mwingine silaha yake.

Kusoma sura kamili Nehemia 4