Agano la Kale

Agano Jipya

Nehemia 4:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Sanbalati aliposikia kuwa tumeanza kazi ya kuujenga upya ukuta, alikasirika sana, akaanza kutukebehi,

2. mbele ya rafiki zake na majeshi ya Wasamaria, akisema, “Hawa Wayahudi wanyonge wanafanya nini? Je, kusudi lao ni kuujenga upya mji? Je, watatoa tambiko? Wanaweza kumaliza kazi kwa siku moja tu? Je, wataweza kufanya mawe yaliyorundikana kwenye takataka na kuteketea, yafae kujengea?”

3. Tobia, Mwamoni, aliyekuwa akisimama karibu naye, alitilia mkazo akisema, “Wanajenga nini? Mbweha akipanda juu yake, atabomoa huo ukuta wao wa mawe!”

4. Ndipo nikamwomba Mungu nikisema, “Ee Mungu wetu, sikia wanavyotukebehi; urudishe dharau yao juu yao wenyewe na uwaache watekwe na kuchukuliwa mateka katika nchi ya kigeni.

5. Kamwe usiwasamehe hatia yao, wala dhambi yao kamwe usiisamehe; kwani wamekukasirisha mbele ya wajenzi.”

6. Lakini tuliendelea na ujenzi wa ukuta mpaka ukafikia nusu yake kwa sababu watu walikuwa wamedhamiria kwa dhati.

7. Lakini Sanbalati, Tobia, Waarabu, Waamoni na Waashdodi waliposikia kuwa ujenzi mpya wa ukuta wa Yerusalemu ulikuwa unasonga mbele na kwamba mapengo katika ukuta yanazibwa barabara, wao walizidi kukasirika.

8. Wakala njama kwa pamoja kuja Yerusalemu kutushambulia na hivyo kuleta mvurugano katika mji huo.

9. Ndipo tulipomwomba Mungu wetu na kuweka ulinzi dhidi yao, mchana na usiku.

10. Watu wa Yuda wakawa wakilalamika wakisema, “Nguvu za vibarua zinapungua na bado kuna takataka nyingi za kubeba. Hatuwezi kuendelea kujenga ukuta.”

11. Nao adui zetu wakawa wanasema, “Hawataweza kujua wala kuona, hadi tutakapofika kwao na kuwaua na kusimamisha kazi.”

12. Wayahudi waliokaa miongoni mwa adui zetu waliposikia maneno yao, walitujia mara kumi wakisema, “Watakuja toka kila mahali wanapokaa na kutushambulia.”

13. Hivyo, kwenye sehemu za chini za ukuta ambazo zilikuwa bado kumalizika, nyuma ya ukuta, katika mahali pa wazi, niliwapanga watu kulingana na jamaa zao wakiwa na mapanga, mikuki na pinde.

Kusoma sura kamili Nehemia 4