Sura

  1. 1
  2. 2
  3. 3
  4. 4
  5. 5
  6. 6
  7. 7
  8. 8
  9. 9
  10. 10
  11. 11
  12. 12
  13. 13
  14. 14
  15. 15
  16. 16
  17. 17
  18. 18
  19. 19
  20. 20
  21. 21
  22. 22
  23. 23
  24. 24
  25. 25
  26. 26
  27. 27
  28. 28
  29. 29
  30. 30
  31. 31
  32. 32
  33. 33
  34. 34
  35. 35
  36. 36
  37. 37
  38. 38
  39. 39
  40. 40
  41. 41
  42. 42
  43. 43
  44. 44
  45. 45
  46. 46
  47. 47
  48. 48
  49. 49
  50. 50

Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 42 Biblia Habari Njema (BHN)

Ndugu za Yosefu wanakwenda Misri

1. Yakobo alipopata habari kwamba kulikuwa na nafaka huko Misri, aliwaambia wanawe, “Mbona mnaketi mkitazamana tu?

2. Nimesikia kwamba Misri kuna nafaka. Nendeni huko mkanunue nafaka tusije tukafa njaa.”

3. Hivyo ndugu kumi wa Yosefu wakaenda Misri kununua nafaka.

4. Lakini Yakobo hakumwacha Benyamini, nduguye Yosefu, aende pamoja nao maana aliogopa kwamba angeweza kupata madhara.

5. Basi, wana wa Israeli wakafika Misri wakiwa miongoni mwa wanunuzi wengine, kwani hata katika nchi ya Kanaani kulikuwa na njaa.

6. Wakati huo Yosefu alikuwa ndiye mkuu huko Misri. Yeye ndiye aliyehusika na kuwauzia wananchi nafaka. Basi, kaka zake wakaja na kumwinamia Yosefu kwa heshima.

7. Yosefu alipowaona kaka zake akawatambua, lakini akajifanya kana kwamba hawafahamu, akasema nao kwa ukali. Akawauliza, “Mmetoka wapi nyinyi?” Wakamjibu, “Tumetoka nchini Kanaani, tumekuja kununua chakula.”

8. Ingawa Yosefu aliwatambua kaka zake, wao hawakumtambua.

9. Akakumbuka ndoto zake za zamani juu ya kaka zake, akawaambia, “Nyinyi ni wapelelezi. Mmekuja kupeleleza udhaifu wa nchi yetu.”

10. Wao wakamjibu, “Sivyo, bwana wetu. Sisi watumishi wako tumekuja kununua chakula.

11. Sisi ni ndugu, wana wa baba mmoja. Sisi ni watu waaminifu, na wala si wapelelezi.”

12. Lakini Yosefu akasisitiza, “Sivyo! Mmekuja hapa ili kupeleleza udhaifu wa nchi yetu.”

13. Wakamwambia, “Sisi, watumishi wako, tuko ndugu kumi na wawili, wana wa mtu mmoja, mwenyeji wa nchi ya Kanaani. Mdogo wetu amebaki na baba nyumbani, na ndugu yetu mwingine ni marehemu.”

14. Lakini Yosefu akawaambia, “Ni kama nilivyosema: Nyinyi ni wapelelezi tu.

15. Hivi ndivyo mtakavyojaribiwa: Naapa kwa jina la Farao, kwamba hamtatoka hapa mpaka mdogo wenu atakapokuja.

16. Mtumeni mmoja wenu akamlete huyo ndugu yenu mdogo, wakati wengine wenu wanamngoja gerezani. Hapo ndipo maneno yenu yatakapojulikana ukweli wake. La sivyo, naapa kwa jina la Farao kwamba nyinyi ni wapelelezi.”

17. Kisha akawatia wote gerezani kwa muda wa siku tatu.

18. Siku ya tatu Yosefu akawaambia, “Kwa kuwa mimi ni mcha Mungu, fanyeni hivi ili mpate kuishi:

19. Kama kweli nyinyi ni watu waaminifu, mmoja wenu na abaki kifungoni, na wengine wawapelekee nafaka jamaa zenu wenye njaa.

20. Kisha mleteni kwangu ndugu yenu mdogo. Hii itathibitisha ukweli wa maneno yenu, nanyi hamtauawa.” Basi, wakakubali kufanya hivyo.

21. Kisha wakasemezana wao kwa wao, “Kweli sisi tulimkosea ndugu yetu. Ingawa tulimwona akisononeka rohoni mwake, sisi hatukumjali hata alipotusihi. Ndiyo maana taabu hii yote inatupata.”

22. Reubeni akawaambia, “Je, mimi sikuwaambieni tusimdhuru kijana? Lakini nyinyi hamkunisikiliza! Sasa tunaadhibiwa kwa ajili ya damu yake.”

23. Wao hawakujua kuwa Yosefu alielewa yote hayo waliyosema, maana alipoongea nao ilikuwa kwa njia ya mkalimani.

24. Yosefu akaenda kando, akaangua kilio. Alipotulia, akarudi kuzungumza nao. Kisha akamkamata Simeoni na kumtia pingu mbele ya macho yao.

Ndugu za Yosefu wanarudi nyumbani

25. Yosefu akatoa amri mifuko yao ijazwe nafaka, kila mmoja wao arudishiwe fedha yake katika gunia lake, na wapewe chakula cha njiani. Wakafanyiwa mambo hayo yote.

26. Wakawatwisha punda wao mizigo yao ya nafaka, wakaondoka.

27. Ikawa walipofika mahali pa kulala wageni huko njiani, mmoja wao akafungua gunia lake ili apate kumlisha punda wake, akashangaa kukuta fedha yake mdomoni mwa gunia lake.

28. Akawaambia ndugu zake, “Fedha yangu imerudishwa. Hii hapa mdomoni mwa gunia langu!” Waliposikia hayo, wakafa moyo. Wakatazamana huku wanatetemeka na kuulizana, “Ni jambo gani hili alilotutendea Mungu?”

29. Walipowasili nchini Kanaani kwa baba yao Yakobo, walimsimulia yote yaliyowapata, wakamwambia,

30. “Mkuu wa nchi ile alisema nasi kwa ukali, na kutushuku kwamba sisi ni wapelelezi nchini mwake.

31. Lakini sisi tulimweleza kuwa sisi ni watu waaminifu, na wala si wapelelezi.

32. Tulimweleza kuwa sisi tuko ndugu kumi na wawili wa baba mmoja, na kwamba mmoja wetu ni marehemu na yule mdogo yuko nyumbani nchini Kanaani pamoja na baba yetu.

33. Ndipo mkuu wa nchi hiyo akatuambia, ‘Hivi ndivyo nitakavyotambua kama kweli nyinyi ni watu waaminifu: Mwacheni kwangu ndugu yenu mmoja, nanyi wengine mpeleke nafaka nyumbani kwa jamaa zenu wenye njaa.

34. Kisha mleteni kwangu huyo ndugu yenu mdogo, na hapo nitajua kuwa nyinyi si wapelelezi, ila ni watu waaminifu. Mkifanya hivyo nitamwacha huru ndugu yenu, nanyi mtaruhusiwa kufanya biashara katika nchi hii.’”

35. Walipokuwa wanamimina nafaka kutoka magunia yao, walishangaa kuona kila mmoja wao amerudishiwa kifuko chake na fedha ndani ya gunia lake. Walipoona hayo, wote pamoja na baba yao, wakashikwa na hofu.

36. Baba yao Yakobo, akawaambia, “Mnanipokonya watoto wangu! Yosefu hayuko; Simeoni hayuko; sasa mnataka kumchukua na Benyamini. Yote hayo yamenipata!”

37. Hapo Reubeni akamwambia baba yake, “Nisipomrudisha Benyamini, waue wanangu wawili. Mwache Benyamini mikononi mwangu, nami nitamlinda na kumrudisha kwako.”

38. Lakini baba yake akamjibu, “Mwanangu hatakwenda nanyi; ndugu yake amekwisha fariki, naye peke yake ndiye aliyebaki. Mimi ni mzee mwenye mvi ikiwa kijana huyu atapatwa na madhara yoyote katika safari mtakayofanya basi, mtaniua kwa huzuni.”