Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 19:18-28 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Loti akawaambia, “La, bwana zangu!

19. Ni kweli kwamba mimi mtumishi wenu nimepata fadhili mbele yenu, nanyi mmenionea huruma sana kwa kuyaokoa maisha yangu; lakini milimani ni mbali mno. Maangamizi haya yatanikuta kabla sijafika huko, nami nitakufa.

20. Tazameni, kule kuna mji mdogo ambao naweza kuukimbilia kwani uko karibu. Basi, mniruhusu nikimbilie huko. Ule ni mji mdogo tu, na huko nitasalimika.”

21. Naye akamjibu, “Sawa, nimekubali ombi lako. Sitauangamiza mji ulioutaja.

22. Harakisha! Kimbilia huko, nami sitafanya lolote mpaka utakapowasili huko.” Hivyo mji huo ukaitwa Soari.

23. Jua lilikuwa limekwisha chomoza wakati Loti alipowasili mjini Soari.

24. Ndipo Mwenyezi-Mungu akateremsha moto mkali wa kiberiti kutoka mbinguni juu ya Sodoma na Gomora,

25. akaiangamiza miji hiyo, bonde lote, wakazi wake wote na mimea yote katika nchi hiyo.

26. Lakini mkewe Loti aliyekuwa nyuma ya Loti, akatazama nyuma, akageuka nguzo ya chumvi.

27. Asubuhi na mapema, Abrahamu alikwenda mahali alipokuwa amesimama mbele ya Mwenyezi-Mungu.

28. Akiwa hapo, akatazama chini pande za Sodoma na Gomora na eneo lote la bondeni, akashangaa kuona moshi ukipanda, moshi kama wa tanuri kubwa.

Kusoma sura kamili Mwanzo 19