Agano la Kale

Agano Jipya

Mwanzo 19:13-25 Biblia Habari Njema (BHN)

13. kwa maana kilio kilichomfikia Mwenyezi-Mungu dhidi ya wakazi wa hapa ni kikubwa mno, naye ametutuma tuje kuwaangamiza.”

14. Basi, Loti akawaendea wachumba wa binti zake, akawaambia, “Haraka! Tokeni mahali hapa, maana Mwenyezi-Mungu atauangamiza mji huu.” Lakini wao wakamwona kama mtu mcheshi tu.

15. Kulipokucha, malaika wakamhimiza Loti wakisema, “Amka, mchukue mkeo na hawa binti zako wawili msije mkaangamia wakati mji huu unapoadhibiwa.”

16. Loti akawa anasitasita. Lakini kwa vile Mwenyezi-Mungu alivyomhurumia Loti, wale malaika wakamshika yeye, mkewe na binti zake wawili, wakamtoa nje ya mji.

17. Walipowatoa nje ya mji, malaika mmoja wao akawaambia, “Kimbieni kwa usalama wenu. Msiangalie nyuma wala kusimama popote bondeni. Kimbilieni milimani, msije mkaangamia.”

18. Loti akawaambia, “La, bwana zangu!

19. Ni kweli kwamba mimi mtumishi wenu nimepata fadhili mbele yenu, nanyi mmenionea huruma sana kwa kuyaokoa maisha yangu; lakini milimani ni mbali mno. Maangamizi haya yatanikuta kabla sijafika huko, nami nitakufa.

20. Tazameni, kule kuna mji mdogo ambao naweza kuukimbilia kwani uko karibu. Basi, mniruhusu nikimbilie huko. Ule ni mji mdogo tu, na huko nitasalimika.”

21. Naye akamjibu, “Sawa, nimekubali ombi lako. Sitauangamiza mji ulioutaja.

22. Harakisha! Kimbilia huko, nami sitafanya lolote mpaka utakapowasili huko.” Hivyo mji huo ukaitwa Soari.

23. Jua lilikuwa limekwisha chomoza wakati Loti alipowasili mjini Soari.

24. Ndipo Mwenyezi-Mungu akateremsha moto mkali wa kiberiti kutoka mbinguni juu ya Sodoma na Gomora,

25. akaiangamiza miji hiyo, bonde lote, wakazi wake wote na mimea yote katika nchi hiyo.

Kusoma sura kamili Mwanzo 19