Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 15:11-27 Biblia Habari Njema (BHN)

11. “Ewe Mwenyezi-Mungu,ni nani kati ya miungu anayelingana nawe?Ni nani aliye kama wewe uliye mtakatifu mkuu,utishaye kwa matendo matukufu,unayetenda mambo ya ajabu?

12. Uliunyosha mkono wako wa kulia,nayo nchi ikawameza maadui zetu.

13. “Kwa fadhili zako kuu umewaongoza watu uliowakomboa,kwa nguvu yako umewaongoza kwenye makao yako matakatifu.

14. Watu wa mataifa wamesikia hayo wakatetemeka;wakazi wa Filistia wamekumbwa na kitisho.

15. Wakuu wa Edomu wamefadhaishwa;viongozi wa Moabu wamekumbwa na woga mkuu;wakazi wote wa Kanaani wamevunjika moyo.

16. Kitisho na hofu vimewavamia.Kwa sababu ya ukuu wa nguvu zako,wao wamenyamaza kimya kama jiwe,mpaka watu wako ee Mwenyezi-Mungu, wapite,naam, mpaka watu hao uliowakomboa wamewapita.

17. Wewe utawaleta watu wako na kuwapanda mlimani pako;pale ulipochagua ee Mwenyezi-Mungu pawe makao yako,mahali patakatifu ee Mwenyezi-Mungu ulipojenga kwa mikono yako.

18. Wewe, ee Mwenyezi-Mungu,watawala milele na milele.”

19. Wakati farasi wa Farao na magari yake pamoja na wapandafarasi wake walipoingia mahali pakavu baharini, Mwenyezi-Mungu aliyarudisha maji ya bahari yakawafunika. Lakini Waisraeli waliendelea kutembea pakavu katikati ya bahari.

20. Basi nabii Miriamu, dada yake Aroni, akachukua kingoma mkononi, na wanawake wengine wote wakamfuata wakiwa na vingoma vyao wakicheza.

21. Miriamu akawaongoza kwa kuimba,“Mwimbieni Mwenyezi-Mungu kwani ameshinda kwa fahari,farasi na mpandafarasi wake amewatosa baharini.”

22. Kisha, Mose aliwaongoza Waisraeli kutoka bahari ya Shamu, wakaenda mpaka jangwa la Shuri. Walisafiri kwa muda wa siku tatu jangwani bila kuona maji yoyote.

23. Walipofika mahali panapoitwa Mara, hawakuweza kuyanywa maji ya Mara kwa sababu yalikuwa machungu. Kwa sababu hiyo mahali hapo pakaitwa Mara.

24. Basi, watu wote wakamlalamikia Mose wakisema, “Sasa tutakunywa nini?”

25. Hapo Mose akamlilia Mwenyezi-Mungu, naye akamwonesha kipande cha mti, na Mose akakitumbukiza katika maji; maji hayo yakawa mazuri.Huko Mungu aliwapa Waisraeli amri na agizo, ili ajue uthabiti wao,

26. akawaambia, “Ikiwa mtaisikiliza kwa makini sauti yangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kutenda yaliyo sawa mbele yangu, na kuheshimu amri na maagizo yangu yote, basi, mimi sitawaletea yale magonjwa niliyowaletea Wamisri. Kwa sababu, mimi ndimi Mwenyezi-Mungu ninayewaponya nyinyi.”

27. Kisha Waisraeli wakawasili huko Elimu ambako kulikuwa na chemchemi kumi na mbili na mitende sabini. Wakapiga kambi yao huko karibu na maji.

Kusoma sura kamili Kutoka 15