Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 14:20-31 Biblia Habari Njema (BHN)

20. ukakaa katikati ya Waisraeli na Wamisri. Lile wingu likawatia Wamisri giza, lakini likawaangazia Waisraeli usiku. Kwa hiyo, makundi hayo mawili, jeshi la Farao na kundi la Waisraeli, hayakukaribiana usiku kucha.

21. Mose akaunyosha mkono wake juu ya bahari, naye Mwenyezi-Mungu akaisukuma bahari nyuma kwa upepo mkali toka mashariki. Upepo huo ulivuma usiku kucha, ukaigawa bahari sehemu mbili na katikati kukatokeza nchi kavu.

22. Waisraeli wakapita katikati ya bahari mahali pakavu, kuta za maji zikiwa upande wao wa kulia na wa kushoto.

23. Wamisri wakawafuata kwa kupitia nchi kavu iliyokuwa katikati ya bahari pamoja na farasi wao, magari yao ya vita na wapandafarasi wao wote.

24. Karibu na mapambazuko, Mwenyezi-Mungu aliliangalia jeshi la Wamisri kutoka katika ule mnara wa moto na ule mnara wa wingu, akalitia hofu kubwa.

25. Aliyakwamisha magurudumu ya magari yao, yakawa yakienda kwa shida sana. Hapo Wamisri wakasema, “Tuwakimbie Waisraeli; Mwenyezi-Mungu anawapigania Waisraeli dhidi yetu.”

26. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi na kuwafunika Wamisri pamoja na magari yao na wapandafarasi wao.”

27. Basi, Mose akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka bahari ikarudia hali yake ilivyokuwa. Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji lakini Mwenyezi-Mungu akawasukumizia baharini.

28. Maji yakayafunika magari pamoja na wapandafarasi; jeshi lote la Farao lililokuwa limewafuatia Waisraeli likafa baharini. Hakunusurika Mmisri hata mmoja.

29. Lakini Waisraeli walipita katikati ya bahari mahali pakavu, kuta za maji zikiwa zimesimama upande wao wa kulia na wa kushoto.

30. Siku hiyo Mwenyezi-Mungu aliwaokoa Waisraeli mikononi mwa Wamisri; nao Waisraeli wakawaona Wamisri wamelala ufuoni wamekufa.

31. Waisraeli walipoona tendo hilo la ajabu alilofanya Mwenyezi-Mungu dhidi ya Wamisri, wakamcha, wakawa na imani na Mwenyezi-Mungu na Mose mtumishi wake.

Kusoma sura kamili Kutoka 14