Agano la Kale

Agano Jipya

Kutoka 14:11-28 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Wakamwambia Mose, “Je, hapakuwa na makaburi ya kutosha nchini Misri hata ukatuleta tufie huku jangwani? Mbona umetutendea haya, kwa tututoa katika nchi ya Misri?

12. Je, hatukukuambia mambo haya tulipokuwa bado Misri? Tulikuambia utuache tuendelee kuwatumikia Wamisri. Ingalikuwa afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufia huku jangwani.”

13. Mose akawaambia Waisraeli, “Msiogope! Kaeni imara! Leo mtaona jinsi Mwenyezi-Mungu atakavyowaokoa. Maana, hawa Wamisri mnaowaona leo, hamtawaona tena.

14. Mwenyezi-Mungu atawapigania; nyinyi mnachotakiwa kufanya ni kutulia tu.”

15. Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Kwa nini mnanililia? Waambie Waisraeli waendelee mbele.

16. Inua fimbo yako na kuinyosha juu ya bahari. Maji yatagawanyika na Waisraeli wataweza kuvuka katikati ya bahari mahali pakavu.

17. Mimi nitawafanya Wamisri kuwa wakaidi, nao watawafuatia katikati ya bahari; nami nitajipatia utukufu kutokana na kuangamizwa kwa Farao na jeshi lake, magari yake ya vita pamoja na wapandafarasi wake.

18. Naam, nitatukuka kwa kumwangamiza Farao na jeshi lake, pamoja na magari yake na wapandafarasi; nao Wamisri watajua kwamba mimi ndimi Mwenyezi-Mungu.”

19. Basi, malaika wa Mungu aliyekuwa mbele ya kundi la Waisraeli aliondoka akakaa nyuma yao. Na ule mnara wa wingu pia uliondoka mbele ukasimama nyuma yao,

20. ukakaa katikati ya Waisraeli na Wamisri. Lile wingu likawatia Wamisri giza, lakini likawaangazia Waisraeli usiku. Kwa hiyo, makundi hayo mawili, jeshi la Farao na kundi la Waisraeli, hayakukaribiana usiku kucha.

21. Mose akaunyosha mkono wake juu ya bahari, naye Mwenyezi-Mungu akaisukuma bahari nyuma kwa upepo mkali toka mashariki. Upepo huo ulivuma usiku kucha, ukaigawa bahari sehemu mbili na katikati kukatokeza nchi kavu.

22. Waisraeli wakapita katikati ya bahari mahali pakavu, kuta za maji zikiwa upande wao wa kulia na wa kushoto.

23. Wamisri wakawafuata kwa kupitia nchi kavu iliyokuwa katikati ya bahari pamoja na farasi wao, magari yao ya vita na wapandafarasi wao wote.

24. Karibu na mapambazuko, Mwenyezi-Mungu aliliangalia jeshi la Wamisri kutoka katika ule mnara wa moto na ule mnara wa wingu, akalitia hofu kubwa.

25. Aliyakwamisha magurudumu ya magari yao, yakawa yakienda kwa shida sana. Hapo Wamisri wakasema, “Tuwakimbie Waisraeli; Mwenyezi-Mungu anawapigania Waisraeli dhidi yetu.”

26. Kisha Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu ya bahari, ili maji yarudi na kuwafunika Wamisri pamoja na magari yao na wapandafarasi wao.”

27. Basi, Mose akaunyosha mkono wake juu ya bahari, na kulipopambazuka bahari ikarudia hali yake ilivyokuwa. Wamisri wakajaribu kuyakimbia maji lakini Mwenyezi-Mungu akawasukumizia baharini.

28. Maji yakayafunika magari pamoja na wapandafarasi; jeshi lote la Farao lililokuwa limewafuatia Waisraeli likafa baharini. Hakunusurika Mmisri hata mmoja.

Kusoma sura kamili Kutoka 14