Agano la Kale

Agano Jipya

Kumbukumbu La Sheria 30:11-20 Biblia Habari Njema (BHN)

11. “Amri ninazowapa leo si ngumu mno kwenu, wala haziko mbali nanyi.

12. Haziko mbinguni hata mseme, ‘Nani atakayepanda juu mbinguni kutuletea ili tupate kuzisikia na kuzitii?’

13. Wala haziko ngambo ya bahari, hata mseme, ‘Nani atakayevuka bahari atuletee ili tuzisikie na kuzitii.’

14. Sivyo, ila zipo karibu nanyi, vinywani mwenu na mioyoni mwenu, mpate kuzitekeleza.

15. “Leo hii nawapeni uchaguzi kati ya mema na mabaya; kati ya uhai na kifo.

16. Kama mkitii amri za Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, ambazo ninawapa leo, mkampenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, na kufuata njia zake na kushika masharti na maagizo yake, basi, mtaishi na kuongezeka; naye Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, atawabariki katika nchi ambayo mnakwenda kuimiliki.

17. Lakini mkipotoshwa na kukataa kumsikiliza, mkavutwa kuabudu miungu mingine na kuitumikia,

18. mimi nawatangazieni leo hii kwamba mtaangamia. Hamtaishi kwa muda mrefu katika nchi mnayokwenda kuimiliki, ngambo ya mto wa Yordani.

19. Naziita mbingu na dunia zishuhudie juu yenu leo hii, kwamba nimewapeni uchaguzi kati ya uhai na kifo, kati ya baraka na laana. Basi, chagueni uhai nyinyi na wazawa wenu mpate kuishi,

20. mkimpenda Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, mkiitii sauti yake na kuambatana naye. Maana kufanya hivyo kunamaanisha kwamba mtapata maisha marefu na kuishi katika nchi ambayo Mwenyezi-Mungu aliwaahidi wazee wenu, Abrahamu, Isaka na Yakobo, kwamba atawapeni.”

Kusoma sura kamili Kumbukumbu La Sheria 30