Agano la Kale

Agano Jipya

Isaya 44:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. “Sikiliza ewe taifa Israeli mtumishi wangu;sikiliza ewe kizazi cha Yakobo mteule wangu.

2. Mimi, Mwenyezi-Mungu Muumba wako,niliyekufanya tangu tumboni mwa mama yako,nimekuja kukusaidia wewe.Mimi Mwenyezi-Mungu nasema:Usiogope, ewe taifa la Yakobo, mtumishi wangu,naam, usiogope ewe Yeshuruni mteule wangu.

3. “Nitaimwagilia maji nchi iliyokauka,na kutiririsha mto katika nchi kame.Nitawamiminia roho yangu wazawa wako,nitawamwagia watoto wako baraka yangu.

4. Watachipua kama nyasi penye maji mengi,kama majani kandokando ya vijito.

5. “Mmoja atasema: ‘Mimi ni wa Mwenyezi-Mungu’,mwingine atajiita kwa jina la Yakobo,mwingine ataandika mkononi mwake, ‘Wa Mwenyezi-Mungu’,na kujitambulisha kwa jina la Israeli.”

6. Mwenyezi-Mungu, Mfalme na Mkombozi wa Israeli,naam, Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi:“Mimi ni wa kwanza na wa mwisho;hakuna Mungu mwingine ila mimi.

7. Ni nani Mungu aliye kama mimi?Mwache atangaze na kusema wazi mbele yangu.Nani alitangaza hapo kale mambo ambayo yatatukia?Na watuambie yale ambayo bado kutokea.

8. Enyi watu wangu, msiogope wala msiwe na hofu,Je, sikuwaambia tangu zamani mambo yatakayotokea?Nyinyi ni mashahidi wangu.Je, yuko Mungu mwingine ila mimi?Je, kuna mwenye nguvu mwingine?Huyo simjui!”

9. Watu wote wanaotengeneza sanamu za miungu ni bure kabisa; na vitu hivyo wanavyovifurahia haviwafai chochote. Wanaoshuhudia hiyo miungu ya uongo ni vipofu na wajinga. Kwa hiyo hao wataaibishwa!

10. Ajabu ya mtu kutengeneza sanamu au kinyago cha mungu ambaye hawezi kumsaidia chochote!

11. Hakika wote wanaomheshimu wataaibishwa, tena hao mafundi wa sanamu ni binadamu tu. Basi, wakutane wote, wajitokeze, nao watatishika na kuaibishwa.

12. Mfuachuma huchukua madini, akayayeyusha motoni na kufua sanamu. Huigongagonga kwa nyundo ili kuipa umbo kwa mikono yake yenye nguvu. Wakati wote huo yeye huona njaa na kuchoka; huona kiu na nguvu kumwishia.

13. Kadhalika naye seremala hupima kipande cha mbao, akakitia alama kwa kalamu yake, kisha kwa vifaa vyake hukichonga na kukipa umbo la binadamu na sura ya kupendeza; kisha akaiweka sanamu hiyo ya mungu mahali pake pa pekee.

Kusoma sura kamili Isaya 44