Agano la Kale

Agano Jipya

Isaya 10:6-24 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Nilimtuma kuliadhibu taifa ovu,nilimwamuru kuwaadhibu watu niliowakasirikia,kuwapora na kuteka nyara,na kuwakanyaga chini kama tope njiani.

7. Lakini Ashuru hakudhamiria hivyo,yeye alikuwa na nia nyingine;alikusudia kuharibu kabisa,kuangamiza mataifa mengi iwezekanavyo.

8. Maana alisema:“Je, si kweli majemadari wangu ni wafalme?

9. Je, si kweli kwamba Kalno nitautenda kama Karkemishi,mji wa Hamathi kama mji wa Arpadi,Samaria kama Damasko?

10. Kama nimefaulu kuunyosha mkono wangudhidi ya falme zenye sanamu za miungukubwa kuliko sanamu za Yerusalemu na Samaria;

11. je, nitashindwa kuutenda Yerusalemu na sanamu zake,kama nilivyoutenda Samaria na sanamu zake?”

12. Wakati Mwenyezi-Mungu atakapomaliza kazi zake zote mlimani Siyoni na mjini Yerusalemu, atamwadhibu mfalme wa Ashuru, kwa sababu ya majivuno na kiburi chake.

13. Maana mfalme wa Ashuru alisema:“Kwa nguvu zangu mwenyewe nimetenda hayo,na kwa hekima yangu, maana mimi ni mwerevu!Nimeondoa mipaka kati ya mataifa,nikazipora hazina zao;kama fahali nimewaporomosha walioketia viti vya enzi.

14. Kama mtu anyoshaye mkono kwenye kiota,ndivyo nilivyochukua mali yao;kama mtu aokotavyo mayai yaliyoachwa kiotani,ndivyo nilivyowaokota duniani kote,wala hakuna mtu aliyeweza kupiga bawa,au aliyefungua kinywa kunipigia kelele.”Lakini Mwenyezi-Mungu asema hivi:

15. “Je, shoka litajigamba dhidi ya anayelitumia?Msumeno waweza kujivuna dhidi ya mwenye kukata nao?Ni kana kwamba fimbo ingeweza kumwinua anayeishika,au mkongojo kumwinua mwenye kuutumia!”

16. Kwa hiyo, Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi,atawaletea askari wao ugonjwa wa kuwakondesha,na fahari yao itateketezwa kama kwa moto.

17. Mungu aliye mwanga wa Israeli atakuwa kama moto,Mtakatifu wa Israeli atakuwa mwali wa motoambao kwa siku moja utateketeza kila kitu:Miiba yake na mbigili zake pamoja.

18. Misitu yake ya fahari na mashamba yake mazuri,Mwenyezi-Mungu atayaangamiza yote;itakuwa kama mtu aliyemalizwa na ugonjwa.

19. Miti itakayobaki msituni mwake itakuwa michache sanahata mtoto mdogo ataweza kuihesabu.

20. Siku ile wazawa wa Yakobo watakaobaki, naam, Waisraeli watakaosalia hawatalitegemea tena taifa lililowaadhibu, bali watamtegemea kabisa Mwenyezi-Mungu, Mtakatifu wa Israeli.

21. Wazawa wa Yakobo wachache watakaobaki watamrudia Mungu Mkuu.

22. Maana, hata kama sasa Waisraeli ni wengi kama mchanga wa pwani, ni wachache tu watakaorudi. Maangamizi yamepangwa yafanyike, nayo yatafanyika kwa haki tupu.

23. Naam! Bwana, Mwenyezi-Mungu wa majeshi, atakamilisha kabisa katika nchi yote jambo aliloamua kutenda.

24. Kwa hiyo, Bwana Mwenyezi-Mungu wa majeshi asema hivi: “Enyi watu wangu mnaokaa Siyoni msiwaogope Waashuru ambao wanawapiga kwa fimbo, wakiinua mikongojo yao dhidi yenu kama walivyofanya Wamisri.

Kusoma sura kamili Isaya 10