Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 18:4-19 Biblia Habari Njema (BHN)

4. Wao watajiunga nawe kazini na kutimiza wajibu wao kikamilifu kuhusu huduma zote za hema, na wala pasiwe na mtu mwingine atakayekukaribia humo.

5. Nyinyi mtafanya huduma za mahali patakatifu na madhabahu, ili ghadhabu yangu isije ikawatokea tena Waisraeli.

6. Ni mimi niliyewachagua ndugu zenu Walawi miongoni mwa Waisraeli kama toleo kwenu. Wao wametengwa kwa ajili yangu mimi Mwenyezi-Mungu, ili watoe huduma katika hema la mkutano.

7. Lakini wewe peke yako na wanao mtatoa huduma zote za kikuhani kwa ajili ya madhabahu na vyote vilivyomo katika mahali patakatifu. Huo ni wajibu wenu, kwa sababu ninawapeni kipawa cha ukuhani. Mtu yeyote asiyestahili atakayevikaribia vyombo vya hema, atauawa.”

8. Mwenyezi-Mungu akamwambia Aroni, “Ninakukabidhi matoleo waliyonipa Waisraeli, vitu vyote vitakatifu walivyonipa: Vitu vyote vilivyowekwa wakfu na Waisraeli. Ninakupa vitu vyote wewe na wazawa wako kuwa fungu lenu, na hiyo ni haki yenu milele.

9. Kati ya vitu vitakatifu kabisa ambavyo haviteketezwi motoni, hivi vitakuwa vyenu: Sadaka za nafaka, sadaka za kuondoa dhambi na sadaka za hatia. Kila kitu watu watakachonitolea kama tambiko takatifu kitakuwa chako na wanao.

10. Mtavila vitu hivyo kama vitu vitakatifu kabisa, na ni wanaume tu ndio watakaovila; vitu hivyo ni vitakatifu kwenu.

11. “Pia, vitu vingine vyote watakavyonitolea Waisraeli kama sadaka za kutikisa, vitakuwa vyako. Ninakupa wewe, wanao na binti zako kuwa haki yenu milele. Mtu yeyote katika jamaa yako asiye najisi anaweza kula vitu hivyo.

12. “Ninakupa vitu vyote vizuri vinavyotokana na malimbuko ambayo Waisraeli hunitolea: Mafuta safi, divai na nafaka.

13. Mazao yote ya kwanza ya matunda mabivu ya mashamba yao ambayo wataniletea mimi, yatakuwa yako. Kila mtu asiye najisi katika jamaa yako anaweza kula.

14. Kila kitu kilichowekwa wakfu nchini Israeli kitakuwa chenu.

15. “Kila mzaliwa wa kwanza ambaye Waisraeli watanitolea, akiwa mzaliwa wa kwanza wa binadamu, au wa mnyama, atakuwa wako. Walakini huna budi kuwakomboa wazaliwa wa kwanza wote wa binadamu, na kila mzaliwa wa kwanza wa mnyama aliye najisi ni lazima akombolewe.

16. Wazaliwa hao wa kwanza watakombolewa wakiwa wenye umri wa mwezi mmoja kwa kulipiwa fedha shekeli tano, kulingana na vipimo vya hema takatifu.

17. Lakini wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe, kondoo au mbuzi wasikombolewe; hao ni watakatifu. Damu yao utainyunyizia madhabahu na mafuta yao utayateketeza kuwa sadaka ya kuteketezwa ambayo ni harufu nzuri inipendezayo mimi Mwenyezi-Mungu.

18. Nyama yao unaweza kuila, kama vile kidari na mguu wa nyuma wa kulia vinavyotolewa kama sadaka ya kutikisa.

19. “Ninakupa wewe, wanao na binti zako, vitu vyote ambavyo watu wa Israeli hunitolea; hivyo ni haki yenu daima. Hili ni agano la milele mbele yangu ambalo ni kwa ajili yako na wazawa wako.”

Kusoma sura kamili Hesabu 18