Agano la Kale

Agano Jipya

Hesabu 10:28-36 Biblia Habari Njema (BHN)

28. Huu basi, ndio utaratibu walioufuata Waisraeli kulingana na makundi yao, kila wakati walipovunja kambi na kuanza kusafiri tena.

29. Mose alimwambia shemeji yake, Hobabu mwana wa Reueli, Mmidiani, mkwe wake, “Sisi tunasafiri kwenda mahali ambapo Mwenyezi-Mungu amesema ‘Nitawapa nyinyi mahali hapo’. Basi, twende pamoja, nasi tutakutendea mema; maana Mwenyezi-Mungu ameahidi kutupa sisi Waisraeli fanaka.”

30. Lakini Hobabu akajibu, “Mimi sitafuatana nanyi; ila nitarudi katika nchi yangu na kwa jamaa zangu.”

31. Mose akamwambia, “Tafadhali usituache, maana wewe unajua mahali tunapoweza kupiga kambi jangwani, na unaweza kuwa kiongozi wetu.

32. Tena ukiandamana nasi chochote chema atakachotutendea Mwenyezi-Mungu, ndicho utakachotendewa nawe pia.”

33. Basi, watu wakasafiri toka Sinai, Mlima wa Mwenyezi-Mungu, mwendo wa siku tatu. Sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu liliwatangulia mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupiga kambi.

34. Kila waliposafiri kutoka kambi moja hadi nyingine, wingu la Mwenyezi-Mungu lilikuwa juu yao mchana.

35. Kila wakati sanduku liliposafiri kwenda mbele, Mose alisema, “Inuka, ee Mwenyezi-Mungu, uwatawanye adui zako, na hao wanaokuchukia uwafanye wakimbie kutoka mbele yako.”

36. Na kila wakati liliposimama, Mose alisema, “Warudie, ee Mwenyezi-Mungu, hawa maelfu na maelfu ya Israeli.”

Kusoma sura kamili Hesabu 10