Agano la Kale

Agano Jipya

Ezra 8:22-35 Biblia Habari Njema (BHN)

22. Ingekuwa aibu kubwa kwangu kumwomba mfalme kikosi cha askari na wapandafarasi wa kutulinda na adui njiani maana nilikuwa nimekwisha mwambia kuwa Mungu wetu huwabariki wote wanaomtafuta, lakini huwachukia na kuwaadhibu wote wanaomwacha.

23. Kwa hiyo tulifunga na kumwomba Mungu atulinde, naye aliyasikia maombi yetu.

24. Halafu kati ya makuhani waliokuwa viongozi nilichagua kumi na wawili: Sherebia, Hashabia pamoja na wenzao kumi.

25. Hawa niliwapimia kwa mizani fedha, dhahabu na vyombo ambavyo mfalme, washauri wake, maofisa wake pamoja na watu wa Israeli walivyokuwa wamevitoa kwa ajili ya sadaka ya nyumba ya Mungu wetu.

26. Hivi ndivyo vitu nilivyowapimia: Fedha tani 22, vyombo 100 vya fedha, uzito wake kilo 70, dhahabu kilo 3400,

27. mabakuli 20 ya dhahabu, uzito wake kilo 8, vyombo viwili vya shaba nzuri iliyongaa yenye thamani kama ya dhahabu.

28. Kisha nikawaambia, “Nyinyi ni wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Kadhalika vyombo ni wakfu na fedha na dhahabu ni matoleo ya hiari kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu.

29. Tafadhali vilindeni na vitunzeni mpaka mtakapovipima mbele ya makuhani wakuu, Walawi na viongozi wa koo za Israeli, huko Yerusalemu katika vyumba vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.”

30. Basi, makuhani na Walawi wakachukua fedha, dhahabu na vyombo vyote walivyopimiwa, ili kuvipeleka mjini Yerusalemu katika nyumba ya Mungu wetu.

31. Mnamo siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza, tulisafiri kutoka mto Ahava, kwenda Yerusalemu. Mungu wetu alikuwa pamoja nasi, akatulinda na maadui na washambuliaji wa njiani.

32. Tulipofika Yerusalemu, tulipumzika kwa muda wa siku tatu.

33. Mnamo siku ya nne, tukiwa ndani ya nyumba ya Mungu wetu, tulipima ile fedha, dhahabu na vile vyombo, kisha tukamkabidhi kuhani Meremothi, mwana wa Uria. Meremothi alikuwa pamoja na Eleazari, mwana wa Finehasi, na Walawi wawili, Yozabadi, mwana wa Yeshua, na Noadia, mwana wa Binui.

34. Kila kitu kilihesabiwa na kupimwa na wakati huo uzito wa kila kitu uliandikwa.

35. Kisha, watu wote waliorudi kutoka uhamishoni walimtolea Mungu wa Israeli sadaka zao za kuteketezwa. Walitoa mafahali 12 kwa ajili ya Israeli yote, kondoo madume 96 na wanakondoo 77; pia walitoa mbuzi 12 kama sadaka ya kuondoa dhambi. Wanyama wote hawa walitolewa kuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Mwenyezi-Mungu.

Kusoma sura kamili Ezra 8