Agano la Kale

Agano Jipya

Ezra 8:16-32 Biblia Habari Njema (BHN)

16. Niliita waje kwangu viongozi tisa: Eliezeri, Arieli, Shemaya, Elnathani, Yaribu, Elnathani, Nathani, Zekaria na Meshulamu, pamoja na waalimu wawili, Yoyaribu na Elnathani.

17. Nikawatuma kwa Ido, kiongozi wa jamii ya watu kule Kasifia, nikimwomba yeye pamoja na wenzake wahudumu wa nyumba ya Mungu, watuletee watu watakaohudumu katika nyumba ya Mungu.

18. Kwa neema yake Mungu, walituletea Sherebia, mtu mwenye busara na Mlawi wa ukoo wa Mahli, pamoja na wanawe na ndugu zake kumi na wanane.

19. Walituletea pia Hashabia na Yeshaya, wote wa ukoo wa Merari, pamoja na ndugu zao ishirini.

20. Mbali na hao, kulikuwa na wahudumu wa hekalu 220 ambao babu zao walikuwa wamechaguliwa na mfalme Daudi na maofisa wake kuwasaidia Walawi. Majina ya watu wote hawa yaliorodheshwa.

21. Kisha, nilitoa maagizo kuwa sote tufike karibu na mto Ahava ili tufunge na kujinyenyekeza mbele za Mungu wetu na kumwomba atulinde na kutuongoza katika safari yetu pamoja na watoto wetu.

22. Ingekuwa aibu kubwa kwangu kumwomba mfalme kikosi cha askari na wapandafarasi wa kutulinda na adui njiani maana nilikuwa nimekwisha mwambia kuwa Mungu wetu huwabariki wote wanaomtafuta, lakini huwachukia na kuwaadhibu wote wanaomwacha.

23. Kwa hiyo tulifunga na kumwomba Mungu atulinde, naye aliyasikia maombi yetu.

24. Halafu kati ya makuhani waliokuwa viongozi nilichagua kumi na wawili: Sherebia, Hashabia pamoja na wenzao kumi.

25. Hawa niliwapimia kwa mizani fedha, dhahabu na vyombo ambavyo mfalme, washauri wake, maofisa wake pamoja na watu wa Israeli walivyokuwa wamevitoa kwa ajili ya sadaka ya nyumba ya Mungu wetu.

26. Hivi ndivyo vitu nilivyowapimia: Fedha tani 22, vyombo 100 vya fedha, uzito wake kilo 70, dhahabu kilo 3400,

27. mabakuli 20 ya dhahabu, uzito wake kilo 8, vyombo viwili vya shaba nzuri iliyongaa yenye thamani kama ya dhahabu.

28. Kisha nikawaambia, “Nyinyi ni wakfu kwa Mwenyezi-Mungu. Kadhalika vyombo ni wakfu na fedha na dhahabu ni matoleo ya hiari kwa Mwenyezi-Mungu, Mungu wa babu zenu.

29. Tafadhali vilindeni na vitunzeni mpaka mtakapovipima mbele ya makuhani wakuu, Walawi na viongozi wa koo za Israeli, huko Yerusalemu katika vyumba vya nyumba ya Mwenyezi-Mungu.”

30. Basi, makuhani na Walawi wakachukua fedha, dhahabu na vyombo vyote walivyopimiwa, ili kuvipeleka mjini Yerusalemu katika nyumba ya Mungu wetu.

31. Mnamo siku ya kumi na mbili ya mwezi wa kwanza, tulisafiri kutoka mto Ahava, kwenda Yerusalemu. Mungu wetu alikuwa pamoja nasi, akatulinda na maadui na washambuliaji wa njiani.

32. Tulipofika Yerusalemu, tulipumzika kwa muda wa siku tatu.

Kusoma sura kamili Ezra 8