Agano la Kale

Agano Jipya

Ezra 7:6-16 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Ezra aliondoka Babuloni, yeye alikuwa mwandishi mwenye ujuzi mwingi sana katika sheria ambayo Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, alikuwa amempatia Mose. Na kwa msaada wa Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, mfalme alimpatia Ezra kila kitu alichohitaji.

7. Mnamo mwaka wa saba wa utawala wa mfalme Artashasta, Ezra alifunga safari kutoka Babuloni kwenda Yerusalemu. Baadhi ya watu wa Israeli, makuhani, Walawi, waimbaji, walinda malango na wahudumu wa hekalu walikwenda pamoja naye.

8. Waliwasili mjini Yerusalemu mnamo siku ya kwanza ya mwezi wa tano katika mwaka wa saba wa utawala wa mfalme Artashasta.

9. Mwenyezi-Mungu aliifanikisha sana safari yao waliyokuwa wameianza siku ya kwanza ya mwezi wa kwanza.

10. Ezra alikuwa amejitoa kwa moyo wote kujifunza sheria ya Mwenyezi-Mungu, kuitii na kuwafundisha watu wa Israeli maagizo na amri zake.

11. Ifuatayo ni barua ambayo Artashasta alimpa Ezra, kuhani na mwandishi, na mwenye ujuzi katika amri na masharti ambayo Mwenyezi-Mungu aliwapa watu wa Israeli.

12. “Kutoka kwa Artashasta, mfalme wa wafalme, kwa Ezra, kuhani na mtu mwenye ujuzi katika sheria ya Mungu wa mbinguni; Wasalaam!”

13. “Ninaamuru kwamba katika utawala wangu, Mwisraeli yeyote, au kuhani wao, au Mlawi, akitaka kurudi Yerusalemu kwa hiari yake, anaweza kwenda pamoja nawe.

14. “Mimi pamoja na washauri wangu saba, tunakutuma uende ufanye uchunguzi huko Yuda na Yerusalemu kuona kama sheria ya Mungu wako ambayo umekabidhiwa inafuatwa kikamilifu.

15. Utachukua fedha na dhahabu ambayo mimi na washauri wangu tumemtolea kwa hiari Mungu wa Israeli ambaye hekalu lake limo mjini Yerusalemu.

16. Utachukua pia fedha na dhahabu yote utakayokusanya katika mkoa wote wa Babuloni, pamoja na matoleo ya hiari waliyotoa Waisraeli na makuhani wao kwa ajili ya nyumba ya Mungu wao iliyoko Yerusalemu.

Kusoma sura kamili Ezra 7