Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 40:1-13 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Mwaka wa ishirini na tano tangu kuhamishwa kwetu, siku ya kumi ya mwezi wa kwanza, siku hiyo niliusikia uzito wa nguvu ya Mwenyezi-Mungu. Ilikuwa mwaka wa kumi na nne tangu mji wa Yerusalemu ulipotekwa.

2. Basi, nikiwa katika njozi Mwenyezi-Mungu alinichukua mpaka nchini Israeli, akaniweka juu ya mlima mrefu sana, na upande wa kusini kulikuwa na majengo yaliyoonekana kama mji.

3. Basi, alinipeleka huko, nami nikamwona mtu aliyeonekana anangara kama shaba. Mikononi mwake mtu huyo alikuwa na kamba ya kitani ya kupimia pamoja na ufito wa kupimia, naye alikuwa amesimama karibu na lango.

4. Basi, akaniambia: “Wewe mtu! Tazama vizuri na kusikiliza kwa makini. Zingatia kwa moyo uone kila kitu nitakachokuonesha maana umeletwa hapa ili nikuoneshe kitu. Unapaswa kuwatangazia watu wa Israeli kila kitu utakachoona.”

5. Basi, huko, niliona hekalu nalo lilikuwa limezungukwa na ukuta upande wa nje. Yule mtu akauchukua ufito wake wa kupimia ambao ulikuwa na urefu wa mita 3, akaupima ule ukuta. Ukuta huo ulikuwa na kimo cha mita 3 na unene wa mita 3.

6. Kisha, akaenda kwenye lango la mashariki akapanda ngazi na akiwa juu akapima kizingiti cha lango ambacho kilikuwa na kina mita 3.

7. Kulikuwa na vyumba vya walinzi kila upande wa nafasi ya kupitia na kila kimoja kilikuwa cha mraba: Urefu mita 3 upana mita 3. Kuta zilizotenganisha vyumba hivyo zilikuwa na unene mita 2.5. Kulikuwa na ukumbi mrefu wa mita 3 ambao ulielekea kwenye chumba kikubwa mkabala na hekalu.

8. Yule mtu akakipima pia chumba hicho, nacho kilikuwa na kina mita 4.

9. Halafu akapima kuta zake za nje zikaonekana zina unene wa mita moja. Sehemu ya ndani ya lango ilikuwa sehemu iliyokuwa karibu zaidi na hekalu.

10. Kulikuwa na sehemu ya kuingilia iliyokuwa na vyumba vitatu vya walinzi, kila upande na vyote vilikuwa na ukubwa uleule; nazo kuta zilizovitenganisha zilikuwa na unene uleule.

11. Kisha, yule mtu akapima upana wa nafasi ya kupitia katika lango. Upana wake ulikuwa mita 6.5. Ukubwa wote wa ukumbi wa katikati wa kupitia ulikuwa mita 5.

12. Mbele ya vyumba vya walinzi ambavyo vilikuwa mraba: Mita 3 kwa 3, kulikuwa na ukuta mfupi kama kizuizi ukiwa na kimo cha sentimita 50 na unene sentimita 50.

13. Yule mtu akapima umbali kutoka ukuta wa nyuma wa chumba kimojawapo hadi kwenye ukuta wa nyuma ya chumba upande wa pili penye nafasi ya kupitia, akapata mitakumi na mbili u nusu.

Kusoma sura kamili Ezekieli 40