Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 33:10-18 Biblia Habari Njema (BHN)

10. “Ewe mtu! Waambie Waisraeli jambo hili: Nyinyi mwasema, ‘Tumezidiwa na makosa na dhambi zetu. Tunadhoofika kwa sababu yake! Tutawezaje basi, kuishi?’

11. Basi, waambie: Kama niishivyo mimi Bwana Mwenyezi-Mungu naapa kwamba, mimi sikifurahii kifo cha mtu mwovu, bali napenda mtu mwovu aachane na mwenendo wake mbaya, apate kuishi. Tubuni, achaneni na mwenendo wenu mbaya, enyi Waisraeli! Kwa nini mwataka kufa?

12. “Basi, ewe mtu, waambie wananchi wenzako hivi: Mtu mwadilifu akitenda uovu, uadilifu wake hautamwokoa. Na mtu mwovu akiacha kutenda dhambi hataadhibiwa. Mtu mwadilifu akianza kutenda dhambi uadilifu wake hautamsalimisha.

13. Mimi namwahidi mwadilifu kwamba ataishi; lakini yeye akiamini kwamba uadilifu wake watosha, akaanza kutenda uovu, matendo yake yote mema ya hapo awali hayatakumbukwa; atakufa kwa uovu wake.

14. Tena, nikimwambia mtu mwovu kuwa hakika atakufa naye akaiacha dhambi yake, akaanza kutenda yaliyo ya haki na sawa, hatakufa;

15. kama akirudisha rehani na kurudisha alichoiba, akafuata kanuni ziletazo uhai bila kutenda uovu, mtu huyo hakika ataishi; hatakufa.

16. Dhambi zake zote alizotenda hapo awali hazitakumbukwa; yeye ametenda yaliyo ya haki na mema; kwa hiyo hakika ataishi.

17. “Lakini wananchi wenzako wasema ati: ‘Anachofanya Mwenyezi-Mungu si sawa!’ Kumbe kwa kweli wao ndio hawafanyi kilicho sawa.

18. Mtu mwadilifu akiacha uadilifu wake, akaanza kutenda uovu, atakufa kwa sababu ya uovu wake.

Kusoma sura kamili Ezekieli 33