Agano la Kale

Agano Jipya

Ezekieli 18:10-22 Biblia Habari Njema (BHN)

10. “Ikiwa mtu huyo ana mtoto mkatili au muuaji,

11. mtoto huyo ambaye anafanya mabaya asiyofanya baba yake: Anakula tambiko zilizokatazwa huko mlimani, anamnajisi mke wa jirani yake,

12. anawadhulumu maskini na fukara, anaiba, harudishi rehani, anaziabudu sanamu za miungu na kufanya machukizo,

13. anakopesha kwa riba na kujitafutia ziada, je, mtoto huyo ataishi? La, hataweza kuishi. Kwa kuwa amefanya machukizo yote hayo, hakika atakufa, na yeye mwenyewe atawajibika kwa kifo chake.

14. “Lakini kama mtu huyo akiwa na mtoto ambaye ameona dhambi alizotenda baba yake, lakini yeye hatendi mabaya hayo,

15. hali tambiko zilizokatazwa huko mlimani, wala kuziabudu sanamu za miungu ya Waisraeli, hamnajisi mke wa jirani yake,

16. hampunji mtu yeyote, hashiki rehani, hanyanganyi watu mali zao, bali huwapa chakula wenye njaa na kumvalisha aliye uchi,

17. huepa kutenda uovu, hakopeshi kwa riba, wala kujitafutia ziada, huzifuata amri na maagizo yangu; huyo hatakufa kwa sababu ya uovu wa baba yake. Huyo ataishi.

18. Lakini baba yake, kwa sababu alitoza bei isiyo halali na kumwibia ndugu yake, wala hakuwatendea ndugu zake wema, hakika atakufa kwa sababu ya uovu wake.

19. “Lakini mnauliza, ‘Kwa nini mtoto asiadhibiwe kwa sababu ya dhambi za baba yake?’ Mtoto akitenda yaliyo ya haki na sawa, kama akiwa mwangalifu kuzingatia kanuni zangu zote, basi, huyo hakika ataishi.

20. Atakayetenda dhambi ndiye atakayekufa. Mtoto hatawajibika kwa uovu wa baba yake, wala baba hatawajibika kwa uovu wa mtoto wake. Uadilifu wa mwadilifu utamfaa yeye mwenyewe: Na uovu wa mwovu ataubeba yeye mwenyewe.

21. “Kama mtu mwovu akiachana na dhambi zake zote alizotenda, kama akishika kanuni zangu zote, akatenda yaliyo ya haki na sawa, huyo hakika ataishi, hatakufa.

22. Makosa yake yote aliyofanya hayatakumbukwa; kwa sababu ya uadilifu wake ataishi.

Kusoma sura kamili Ezekieli 18