Agano la Kale

Agano Jipya

Esta 8:7-14 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, yule Myahudi, “Tazameni! Nimempa Esta mali yake Hamani, naye wamekwisha mnyonga kwa sababu ya njama zake dhidi ya Wayahudi.

8. Mwaweza kuwaandikia Wayahudi lolote mpendalo. Tena mwaweza kuandika kwa jina langu na kutumia mhuri wa kifalme, kwa sababu tangazo ambalo limetolewa kwa jina la mfalme na kupigwa mhuri wa mfalme, haliwezi kubatilishwa.”

9. Basi, mnamo siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu uitwao Siwani, Mordekai aliwaita makatibu wote wa mfalme, akawaagiza waandike barua kwa Wayahudi na wakuu, watawala na maofisa wa mikoa yote 127, kuanzia India mpaka Kushi. Nyaraka hizo ziliandikwa kwa kila mkoa katika lugha yake na hati yake ya maandishi, hali kadhalika kwa Wayahudi.

10. Mordekai alikuwa ameandika nyaraka hizo kwa jina la mfalme Ahasuero, akazipiga mhuri kwa pete ya mfalme. Na waliozipeleka walikuwa matarishi waliopanda farasi wenye nguvu waendao kasi.

11. Kwa njia ya nyaraka hizi mfalme aliwaruhusu Wayahudi katika kila mji kukusanyika ili kuyalinda maisha yao. Walikuwa na ruhusa ya kuharibu, kuua bila huruma na kuangamiza kundi lolote la watu au mkoa, lenye kuwashambulia kwa silaha pamoja na wanawake na watoto wao, na kuziteka nyara mali zao.

12. Jambo hili lingefanyika katika mikoa yote ya mfalme Ahasuero, mnamo siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani Adari.

13. Nakala za tangazo hili ambalo lilitolewa kama sheria katika kila mkoa zilisambazwa kwa kila mtu katika kila mkoa, ili Wayahudi wajiandae kulipiza kisasi siku hiyo ifikapo.

14. Kwa amri ya mfalme, matarishi waliopanda farasi wenye nguvu waendao kasi, waliondoka mbio. Tangazo hili pia lilitolewa katika mji mkuu, Susa.

Kusoma sura kamili Esta 8