Agano la Kale

Agano Jipya

Esta 2:7-14 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Alikuwa na binamu, Esta, ambaye jina lake la Kiebrania lilikuwa Hadasa. Esta alikuwa msichana mzuri wa sura na umbo. Wazazi wake walipofariki, Mordekai alimchukua Esta, akamlea kama binti yake.

8. Amri ya mfalme ilipotangazwa hadharani, wasichana wengi walipelekwa Susa, mji mkuu, wakawekwa chini ya ulinzi wa Hegai. Esta naye, alipelekwa kwenye ikulu ya mfalme, akawekwa chini ya uangalizi wa Hegai, yule mwangalizi wa wanawake.

9. Hegai alipendezwa na Esta hata kiasi cha kumpendelea. Bila kupoteza wakati, alimpa Esta mafuta na chakula maalumu. Isitoshe, alimhamishia mahali pazuri kabisa katika nyumba hiyo ya wanawake, akamteulia watumwa wa kike saba kutoka ikulu ya mfalme, wamhudumie.

10. Esta alikuwa hajajitambulisha ukoo wala kabila lake, maana Mordekai alikuwa amemwonya asifanye hivyo.

11. Kila siku Mordekai alipitapita mbele ya ua wa nyumba hiyo ya wanawake ili apate kujua hali ya Esta na mambo ambayo yangempata.

12. Kipindi cha hao wasichana kujiremba na kujitia uzuri kilichukua mwaka mmoja: Miezi sita ya kwanza walitumia mafuta ya manemane, na miezi sita ya mwisho walitumia manukato na mafuta mengineyo. Baada ya hapo, kila mwali, peke yake, alipelekwa kwa mfalme Ahasuero.

13. Wakati wa kwenda kwa mfalme, kila mwali alipewa kila alichotaka kuchukua kutoka nyumba ya wanawake kwenda nacho ikulu.

14. Jioni ulikuwa ndio wakati wa kwenda, na kesho yake asubuhi, mwali huyo alipelekwa katika nyumba nyingine ya wanawake, chini ya Shaashgazi, towashi msimamizi wa masuria wa mfalme. Mwali haikumpasa kurudi kwa mfalme, isipokuwa kama mfalme amependezwa naye kiasi cha kuagiza aitwe kwa jina.

Kusoma sura kamili Esta 2