Agano la Kale

Agano Jipya

Danieli 8:1-15 Biblia Habari Njema (BHN)

1. “Mnamo mwaka wa tatu wa utawala wa mfalme Belshaza, maono mengine yalinijia mimi Danieli, licha ya maono yale ya kwanza.

2. Katika maono haya, nilijikuta niko Susa, mji mkuu wa mkoa wa Elamu. Nilikuwa nimesimama kando ya mto Ulai.

3. Nilipoinua macho yangu, niliona kondoo dume amesimama kando ya mto huo. Kondoo huyo alikuwa na pembe mbili ndefu, lakini moja ilikuwa ndefu zaidi, nayo ilitokea baada ya ile nyingine.

4. Nilimwona huyo kondoo dume akishambulia kuelekea magharibi, kaskazini na kusini. Hakuna mnyama yeyote aliyethubutu kusimama mbele yake, wala kuzikwepa nguvu zake. Alifanya apendavyo na kujikweza mwenyewe.

5. “Nilipokuwa ninawaza juu ya jambo hili, niliona beberu mmoja kutoka upande wa magharibi akija kasi bila kugusa ardhi. Kati ya macho yake alikuwa na pembe moja kubwa sana.

6. Alimwendea yule kondoo dume mwenye pembe mbili niliyemwona akiwa amesimama kando ya mto, akamshambulia kwa nguvu zake zote.

7. Nilimwona akimsogelea yule kondoo dume. Alikuwa amemkasirikia sana yule kondoo dume, hivyo akamshambulia kwa nguvu na kuzivunja zile pembe zake mbili. Yule kondoo dume hakuweza kustahimili. Alibwagwa chini na kukanyagwakanyagwa, wala hapakuwa na yeyote wa kumwokoa katika nguvu zake.

8. Hapo yule beberu alijikweza sana. Lakini alipofikia kilele cha nguvu zake, ile pembe yake kubwa ikavunjika. Badala yake zikaota pembe nne zilizoonekana waziwazi, zikiwa zimeelekea pande nne za pepo.

9. “Katika mojawapo ya pembe hizo nne, paliota upembe mwingine mdogo, ukakua sana kuelekea upande wa kusini-mashariki, na kuelekea nchi ile nzuri mno.

10. Upembe huo ulikua sana kufikia viumbe vya mbinguni; ukaziangusha chini baadhi ya nyota na kuzikanyagakanyaga.

11. Upembe huo ukajikweza juu ya mkuu wa viumbe vya mbinguni. Ukakomesha tambiko za kuteketezwa ambazo mkuu wa viumbe vya mbinguni alitambikiwa kila siku, na kukufuru maskani yake.

12. Viumbe vya mbinguni vikatiwa nguvuni mwake pamoja na tambiko za kuteketezwa kila siku, kwa njia ya upotovu. Nao ukweli ukatupwa chini. Upembe huo ukaibwaga chini ibada ya kweli. Ulifanikiwa katika kila jambo ulilofanya.

13. “Kisha, nikamsikia mtakatifu mmoja akizungumza na mwenzake. Huyo mwenzake alimwuliza, ‘Je, matukio yaliyotangazwa na maono haya yataendelea kwa muda gani? Kwa muda gani sadaka za kuteketezwa za kila siku zitabaki zimebatilishwa? Kwa muda gani upotovu wa kuangamiza kila kitu utaendelea, na mahali patakatifu pamoja na viumbe vya mbingu vitaendelea kukanyagwa?’

14. Yule mtakatifu wa kwanza akamjibu, ‘Kwa muda wa nyakati za jioni na asubuhi 2,300. Kisha maskani ya Mungu itapata tena hali yake halisi.’

15. “Mimi Danieli nilipoyaona hayo maono, na nilipokuwa nikijaribu kujua maana yake, ghafla, mmoja kama mwanaadamu akasimama mbele yangu.

Kusoma sura kamili Danieli 8