Agano la Kale

Agano Jipya

Danieli 2:29-40 Biblia Habari Njema (BHN)

29. Kwako ee mfalme, ulipokuwa umelala kitandani mwako, yalikujia mawazo kuhusu mambo yatakayotukia baadaye; naye Mungu afumbuaye mafumbo, alikuonesha yale yatakayotukia.

30. Lakini mimi sikufumbuliwa fumbo hili kwa sababu nina hekima kuliko wanaadamu wengine, bali ili wewe mfalme, upate kujulishwa maana ya ndoto yako na kujua mawazo yako.

31. “Katika ndoto yako, ee mfalme, uliona sanamu kubwa, yenye nguvu na iliyongaa sana, imesimama mbele yako. Sanamu hiyo ilikuwa ya kutisha mno.

32. Kichwa cha sanamu hiyo kilikuwa cha dhahabu safi, kifua chake na mikono yake vilikuwa vya fedha na tumbo lake na mapaja yake vilikuwa vya shaba.

33. Miguu yake ilikuwa ya chuma na nyayo zake zilikuwa za mchanganyiko wa chuma na udongo wa mfinyanzi.

34. Ukiwa bado unaangalia, jiwe lilingoka lenyewe, bila kuguswa, na kuipondaponda miguu ya shaba na udongo wa mfinyanzi ya ile sanamu, na kuivunja vipandevipande.

35. Mara kile chuma, udongo wa mfinyanzi, shaba, fedha na dhahabu, vyote vikavunjika vipandevipande na kuwa kama makapi ya mahali pa kupuria nafaka wakati wa kiangazi. Upepo ukavipeperushia mbali kisibakie hata kipande kimoja. Lakini lile jiwe lililoivunja ile sanamu likageuka kuwa mlima mkubwa na kuijaza dunia yote.

36. “Hiyo ndiyo ndoto yako, ee mfalme. Na sasa tutakupa maana yake.

37. Wewe, ee mfalme, mfalme wa wafalme! Mungu amekupa ufalme, uwezo, nguvu na utukufu!

38. Amekupa mamlaka juu ya wanaadamu wote, wanyama wa porini na ndege wote wa angani, kokote kule waliko. Wewe ndiwe kile kichwa cha dhahabu!

39. Baada yako utafuata ufalme mwingine, lakini ufalme huo utakuwa dhaifu. Huu utafuatwa na ufalme wa tatu unaofananishwa na shaba; huo utaitawala dunia yote.

40. Baada ya falme hizo, utafuata ufalme mwingine imara kama chuma. Na kama vile chuma kivunjavyo na kupondaponda vitu vyote, ndivyo ufalme huo utakavyovunjavunja na kusagilia mbali falme zilizotangulia.

Kusoma sura kamili Danieli 2