Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 6:24-33 Biblia Habari Njema (BHN)

24. Baadaye, mfalme Ben-hadadi wa Aramu akakusanya jeshi lake lote akatoka na kuuzingira mji wa Samaria.

25. Matokeo yake ilikuwa njaa kali katika mji wa Samaria. Kichwa cha punda kiligharimu vipande themanini vya fedha, na gramu 100 za mavi ya njiwa ziligharimu vipande vitano vya fedha.

26. Siku moja mfalme wa Israeli alipokuwa anatembea juu ya ukuta wa mji, alisikia mwanamke mmoja akimwita, “Nisaidie, ee bwana wangu mfalme!”

27. Mfalme akamwambia, “Mwenyezi-Mungu asipokusaidia, mimi nitakupa msaada kutoka wapi; kutoka katika kiwanja cha kupuria au kutoka katika shinikizo?

28. Shida yako ni nini?” Akamjibu, “Juzi mwanamke huyu alinishauri tumle mwanangu na kesho yake tumle wake.

29. Tukampika mwanangu, tukamla. Kesho yake nikamwambia tumle mwanawe, lakini alikuwa amemficha!”

30. Mara mfalme aliposikia maneno ya mwanamke huyo alirarua nguo zake kwa huzuni, na watu waliokuwa karibu na ukuta waliona kwamba alikuwa amevaa vazi la gunia ndani yake.

31. Naye akasema, “Mungu aniue, Elisha mwana wa Shafati asipokatwa kichwa leo!”

32. Ndipo akatuma mjumbe kwenda kumleta Elisha.Wakati huohuo Elisha alikuwa nyumbani pamoja na wazee waliomtembelea. Kabla ya mjumbe wa mfalme kufika, Elisha akawaambia wazee, “Yule muuaji amemtuma mtu kuja kunikata kichwa! Atakapofika hapa, fungeni mlango, wala msimruhusu aingie. Pia bwana wake anamfuata nyuma.”

33. Kabla hata hajamaliza kusema, mfalme akafika, akasema, “Msiba huu umetoka kwa Mwenyezi-Mungu! Kwa nini niendelee kumngojea tena?”

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 6