Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 6:1-19 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Siku moja, wanafunzi wa manabii walimlalamikia Elisha wakisema, “Mahali hapa tunapokaa ni padogo sana kwetu!

2. Turuhusu twende Yordani tukate miti ili tujijengee mahali patakapotutosha.” Elisha akawajibu, “Nendeni.”

3. Mmoja wao akamwomba akisema, “Tafadhali uwe radhi uende na watumishi wako.” Naye akajibu, “Nitakwenda.”

4. Hivyo akaenda pamoja nao, na walipofika mtoni Yordani wakaanza kukata miti.

5. Mmoja wao alipokuwa anakata miti, shoka lake likachomoka na kuanguka majini; akalia, akisema, “Sasa bwana wangu nitafanya nini? Shoka hili tulikuwa tumeliazima!”

6. Elisha akauliza, “Liliangukia wapi?” Mtu huyo akamwonesha. Elisha akakata kijiti na kukitupa majini na papo hapo shoka likaelea juu ya maji.

7. Elisha akamwamuru alichukue naye akanyosha mkono, akalichukua.

8. Wakati mmoja kulikuwa na hali ya vita kati ya Aramu na Israeli. Basi, mfalme wa Aramu akashauriana na maofisa wake kuhusu mahali watakaposhambulia.

9. Lakini Elisha akampelekea habari mfalme wa Israeli ajihadhari na mahali hapo, kwa kuwa Waaramu walikuwa tayari kupashambulia.

10. Basi, mfalme wa Israeli akapeleka askari wake karibu na mahali alipoambiwa. Elisha aliendelea kumwonya mfalme naye mfalme alijiweka katika hali ya tahadhari. Jambo hilo lilifanyika mara nyingi.

11. Mfalme wa Aramu akafadhaishwa sana na hali hiyo; akawaita maofisa wake, akawauliza, “Niambieni nani kati yenu anayetusaliti kwa mfalme wa Israeli?”

12. Mmoja wao akajibu, “Hakuna anayetusaliti, ee mfalme. Anayehusika ni Elisha, nabii aliyeko huko Israeli. Yeye humwambia mfalme wa Israeli chochote unachosema hata ukiwa katika chumba chako cha kulala.”

13. Mfalme akawaambia, “Nendeni mkapeleleze mjue mahali alipo nami nitawatuma watu wamkamate.” Basi, wakamwarifu kwamba Elisha alikuwa huko Dothani.

14. Kwa hiyo mfalme akapeleka huko jeshi kubwa pamoja na farasi na magari ya kukokotwa. Jeshi hilo likafika huko wakati wa usiku na kuuzingira mji.

15. Mtumishi wa Elisha alipoamka mapema kesho yake na kutoka nje, akaona jeshi pamoja na farasi na magari ya kukokotwa limeuzingira mji. Akarudi ndani akasema, “Ole wetu, ee, Bwana wangu! Sasa tutafanya nini?”

16. Elisha akamjibu, “Usiogope kwa sababu walio pamoja nasi ni wengi kuliko walio pamoja nao.”

17. Kisha Elisha akaomba, “Ee Mwenyezi-Mungu, umfumbue macho ili apate kuona!” Basi, Mwenyezi-Mungu akamfumbua macho huyo kijana, akaona farasi na magari ya moto yakiwa kila mahali katika mlima wote, kumzunguka Elisha.

18. Waaramu waliposhambulia, Elisha alimwomba Mwenyezi-Mungu akisema, “Nakuomba uwafanye watu hawa wawe vipofu!” Mwenyezi-Mungu akasikiliza ombi lake na kuwafanya vipofu.

19. Ndipo Elisha akawaendea na kuwaambia, “Mmepotea njia. Huu siyo mji ambao mnautafuta. Nifuateni nami nitawapeleka kwa yule mnayemtafuta.” Naye akawaongoza mpaka Samaria.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 6