Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 5:7-14 Biblia Habari Njema (BHN)

7. Mfalme wa Israeli aliposoma barua hii alirarua mavazi yake na kusema, “Mbona mfalme wa Aramu anataka nimtibu mtu huyu ukoma wake? Kwani anafikiri mimi ni Mungu aliye na uwezo wa kuua au kufufua? Fahamuni basi, mwone ya kwamba mtu huyu anataka kuniletea mzozo.”

8. Elisha, nabii wa Mungu, alipopata habari kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, alituma ujumbe kwa mfalme, akamwuliza, “Mbona umeyararua mavazi yako? Mlete mtu huyo kwangu, ili apate kujua kwamba kuna nabii katika Israeli?”

9. Naamani akaenda na farasi wake na gari lake mpaka mlangoni mwa Elisha.

10. Elisha akamtuma mtumishi wake amwambie, “Nenda ukaoge mara saba mtoni Yordani, nawe utapona kabisa.”

11. Lakini Naamani alikasirika sana, akaenda zake akisema, “Nilidhani kwamba hakika atanijia na kumwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, apitishe mikono yake juu ya mahali ninapougua na kuniponya!

12. Isitoshe, je, mito Abana na Farpari ya huko Damasko si bora kuliko mito yote ya Israeli? Je, nisingeweza kuoga humo na kupona?” Akaondoka na kurudi nyumbani, huku amekasirika sana.

13. Watumishi wake wakamwendea na kumwambia, “Baba yetu kama nabii angekuambia ufanye jambo fulani gumu, je, hungelifanya? Sasa, aliyokuambia tu ni: ‘Jioshe, ili upone!’”

14. Basi, Naamani akateremka mtoni Yordani akajitumbukiza humo mara saba, kama alivyoagizwa na Elisha mtu wa Mungu, naye akapona kabisa. Ngozi yake ikawa imara na yenye afya kama ya mtoto mdogo.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 5