Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 5:11-21 Biblia Habari Njema (BHN)

11. Lakini Naamani alikasirika sana, akaenda zake akisema, “Nilidhani kwamba hakika atanijia na kumwomba Mwenyezi-Mungu, Mungu wake, apitishe mikono yake juu ya mahali ninapougua na kuniponya!

12. Isitoshe, je, mito Abana na Farpari ya huko Damasko si bora kuliko mito yote ya Israeli? Je, nisingeweza kuoga humo na kupona?” Akaondoka na kurudi nyumbani, huku amekasirika sana.

13. Watumishi wake wakamwendea na kumwambia, “Baba yetu kama nabii angekuambia ufanye jambo fulani gumu, je, hungelifanya? Sasa, aliyokuambia tu ni: ‘Jioshe, ili upone!’”

14. Basi, Naamani akateremka mtoni Yordani akajitumbukiza humo mara saba, kama alivyoagizwa na Elisha mtu wa Mungu, naye akapona kabisa. Ngozi yake ikawa imara na yenye afya kama ya mtoto mdogo.

15. Ndipo akarudi kwa mtu wa Mungu pamoja na watu wake, akasema, “Sasa najua kwamba hakuna Mungu yeyote ila tu Mungu wa Israeli; kwa hiyo, tafadhali sasa upokee zawadi za mtumishi wako.”

16. Elisha akajibu, “Naapa kwa Mwenyezi-Mungu aliye hai ambaye ninamtumikia, kwamba sitapokea zawadi yoyote.”Naamani akamsihi, lakini Elisha akakataa kabisa.

17. Naamani akasema, “Ikiwa hutapokea zawadi zangu, basi tafadhali umpatie mtumishi wako udongo unaoweza kubebwa na nyumbu wawili, kwani toka leo mimi mtumishi wako sitatoa sadaka za kuteketezwa wala tambiko kwa miungu mingine ila tu kwa Mwenyezi-Mungu.

18. Naye Mwenyezi-Mungu na anisamehe ninapofuatana na mfalme wangu kwenda kuabudu katika hekalu la Rimoni mungu wa Aramu. Naomba Mwenyezi-Mungu anisamehe!”

19. Elisha akamwambia, “Nenda kwa amani.” Naamani akaenda zake.Alipokuwa bado hajaenda mbali,

20. Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akasema, “Tazama, bwana wangu amemwachilia Naamani Mwaramu aende bila kupokea chochote alicholeta. Kama Mwenyezi-Mungu aishivyo nitamfuata ili nipate kitu kutoka kwake.”

21. Hapo akaondoka kumfuata Naamani. Naamani alipotazama na kuona mtu anamfuata mbio, akashuka garini mwake akaenda kukutana naye. Basi, akamwuliza, “Je, kuna usalama?”

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 5