Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 3:1-12 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Katika mwaka wa kumi na nane wa utawala wa mfalme Yehoshafati wa Yuda, Yoramu mwana wa Ahabu alianza kutawala Israeli, akatawala kutoka Samaria kwa muda wa miaka kumi na miwili.

2. Yoramu alitenda maovu mbele ya Mwenyezi-Mungu, lakini yeye hakuwa mbaya kama baba na mama yake; maana alibomolea mbali mnara wa Baali uliofanywa na baba yake.

3. Hata hivyo, Yoramu hakuacha dhambi kama mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati aliyemtangulia ambaye alifanya dhambi na kuwafanya watu wa Israeli watende dhambi.

4. Mfalme Mesha wa Moabu alikuwa mfuga kondoo, na kila mwaka alitoa ushuru kwa mfalme wa Israeli wanakondoo laki moja na sufu ya kondoo laki moja.

5. Lakini Ahabu alipofariki, mfalme wa Moabu alimwasi.

6. Kwa hiyo mfalme Yoramu akaondoka Samaria, akakusanya jeshi lote la Israeli.

7. Akatuma ujumbe kwa mfalme Yehoshafati wa Yuda, akamwambia, “Mfalme wa Moabu ameniasi. Je, utashirikiana nami tupigane naye?”Mfalme Yehoshafati akamjibu, “Niko tayari! Mimi na wewe ni kitu kimoja; watu wangu ni kama wako, farasi wangu ni kama wako.

8. Je, tutashambulia kutoka upande gani?” Yoramu akajibu, “Tutashambulia kutoka jangwa la Edomu.”

9. Basi, mfalme Yoramu akaondoka pamoja na mfalme wa Yuda na mfalme wa Edomu. Baada ya kusafiri kwa muda wa siku saba, maji yakawaishia. Hawakuwa na maji kwa majeshi yao wala kwa wanyama wao.

10. Hapo mfalme wa Israeli akasema, “Ole wetu! Mwenyezi-Mungu ametukusanya sote wafalme watatu atutie mikononi mwa mfalme wa Moabu.”

11. Mfalme Yehoshafati akauliza, “Je, hakuna nabii yeyote hapa wa Mwenyezi-Mungu ambaye tunaweza kumwuliza shauri la Mwenyezi-Mungu?” Mtumishi mmoja wa mfalme Yoramu wa Israeli akajibu, “Elisha mwana wa Shafati yupo hapa. Yeye alikuwa mtumishi wa Elia.”

12. Yehoshafati akasema, “Huyo ni nabii wa kweli.” Kisha wafalme hao watatu wakamwendea Elisha.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 3