Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 25:8-21 Biblia Habari Njema (BHN)

8. Katika siku ya saba ya mwezi wa tano wa mwaka wa kumi na tisa wa utawala wa Nebukadneza mfalme wa Babuloni, Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliingia Yerusalemu.

9. Aliichoma moto nyumba ya Mwenyezi-Mungu, ikulu na nyumba zote za Yerusalemu; kila nyumba kubwa aliichoma moto.

10. Nao askari wote wa Wakaldayo waliokuwa pamoja na kapteni na walinzi wa mfalme walizibomoa kuta zilizouzunguka mji wa Yerusalemu.

11. Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme, aliwapeleka uhamishoni watu waliokuwa wamebakia mjini na wale wote waliokuwa wamejisalimisha kwa mfalme wa Babuloni pamoja na watu wengine wote.

12. Lakini aliacha baadhi ya watu waliokuwa maskini kabisa nchini. Aliwaacha watunze mizabibu na kulima mashamba.

13. Wakaldayo walivunja vipandevipande nguzo za shaba ambazo zilikuwa katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, pamoja na vikalio vyake, birika kubwa la shaba nyeusi lililokuwamo katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, wakaichukua shaba nyeusi mpaka Babuloni.

14. Vilevile walichukua vyungu, masepetu, makasi na miiko iliyotumiwa kuchomea ubani na vyombo vingine vyote vya shaba nyeusi vilivyotumiwa katika huduma ya hekalu,

15. wakachukua na vyetezo na mabakuli. Kapteni wa walinzi wa mfalme alipeleka mbali kila chombo cha dhahabu na kila chombo cha fedha.

16. Shaba yote nyeusi aliyotumia Solomoni kutengeneza zile nguzo mbili, birika lile kubwa na vikalio kwa ajili ya nyumba ya Mwenyezi-Mungu haikuweza kupimwa kwa uzito.

17. Kila nguzo ilikuwa na urefu wa mita 8, na juu yake kulikuwa na kichwa cha shaba nyeusi, urefu wa kila kichwa ulikuwa mita 1.25. Kila kichwa kilizungushiwa mapambo ya makomamanga, yote ya shaba nyeusi.

18. Kisha Nebuzaradani kapteni wa walinzi wa mfalme alimchukua mateka Seraya kuhani mkuu, Sefania kuhani wa pili pamoja na maofisa walinda milango watatu;

19. alimchukua towashi mmoja huko mjini ambaye alikuwa akiwaongoza askari vitani, pamoja na watu watano mashuhuri wa mfalme ambao aliwakuta huko. Vilevile, alimchukua katibu wa kamanda mkuu wa jeshi ambaye alitunza kumbukumbu za jeshi pamoja na watu sitini mashuhuri ambao aliwakuta mjini Yerusalemu.

20. Nebuzaradani kapteni wa walinzi aliwachukua watu hao, akawapeleka kwa mfalme wa Babuloni huko Ribla.

21. Mfalme Nebukadneza wa Babuloni aliwapiga na kuwaua watu hao huko Ribla katika nchi ya Hamathi. Hivyo watu wa Yuda walichukuliwa mateka nje ya nchi yao.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 25