Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 23:10-23 Biblia Habari Njema (BHN)

10. Mfalme Yosia pia alipatia najisi mahali pa kuabudia miungu ya uongo palipoitwa Tofethi katika bonde la wana wa Hinomu, ili mtu yeyote asimchome mwanawe au bintiye kuwa tambiko kwa Moleki.

11. Kadhalika aliondoa farasi waliotengwa na wafalme wa Yuda kwa ajili ya jua, kwenye njia ya kuingia katika nyumba ya Mwenyezi-Mungu, karibu na chumba cha Nathan-meleki, kilichokuwa kiungani; naye alichoma kwa moto magari ya jua.

12. Madhabahu ambayo wafalme wa Yuda walijenga paani kwenye chumba cha juu cha Ahazi, pamoja na madhabahu ambayo Manase alijenga katika nyua mbili za nyumba ya Mwenyezi-Mungu aliyabomoa na kuyapondaponda, kisha alitupa mavumbi yake katika kijito cha Kidroni.

13. Mfalme pia alipatia unajisi mahali pa kuabudia palipokuwa upande wa mashariki ya Yerusalemu na kuelekea upande wa mlima wa Ufisadi, mahali mfalme wa Israeli alipopajenga kwa ajili ya Ashtarothi chukizo la Wasidoni, Kemoshi chukizo la Moabu na pia kwa ajili ya Milkomu chukizo la Waamoni.

14. Alivunja nguzo katika vipandevipande; pia alikatakata sanamu za Ashera, na mahali zilipokuwa zinasimama alipajaza mifupa ya watu.

15. Zaidi ya hayo aliharibu huko Betheli mahali pa kuabudia palipojengwa na mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewafanya watu wa Israeli watende dhambi; aliharibu madhabahu hayo na kuvunja mawe yake katika vipandevipande, na kisha akaviponda mpaka vikawa vumbi; pia akachoma sanamu ya Ashera.

16. Kisha Yosia alipogeuka aliona makaburi juu ya kilima; aliagiza mifupa ifukuliwe kutoka makaburini na kuichoma juu ya madhabahu; basi akayatia unajisi madhabahu sawasawa na neno la Mwenyezi-Mungu ambalo mtu wa Mungu alilitangaza, nabii ambaye alitabiri matukio haya.

17. Halafu mfalme aliuliza, “Mnara ninaouona kule ni wa nini?” Nao watu wa mji wakamjibu, “Ni kaburi la mtu wa Mungu ambaye alikuja kutoka Yuda na kutabiri mambo ambayo umeyafanya dhidi ya madhabahu pale Betheli.”

18. Naye akaagiza, “Mwacheni hapo, mtu yeyote asiondoe mifupa yake.” Kwa hiyo waliiacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya nabii aliyetoka Samaria.

19. Katika kila mji wa Samaria mfalme Yosia aliharibu mahali pa kuabudia miungu ya uongo palipojengwa na wafalme wa Israeli, ili kumkashifu Mwenyezi-Mungu. Madhabahu hayo yote aliyaharibu kama vile alivyofanya huko Betheli.

20. Aliwaua makuhani wote wa miungu ya uongo juu ya madhabahu ambapo walitumikia na kuchoma mifupa yao juu ya madhabahu hayo. Kisha alirudi Yerusalemu.

21. Kisha mfalme aliwaamuru watu wote, akisema, “Mfanyieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, Pasaka, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki cha agano.”

22. Hakuna Pasaka iliyosherehekewa kama hii tangu wakati wa waamuzi waliowaamua Waisraeli wala wakati wa ufalme wa Israeli au wa Yuda.

23. Lakini, katika mwaka wa kumi na nane wa enzi ya Yosia, Pasaka ilisherehekewa kwa heshima ya Mwenyezi-Mungu katika Yerusalemu.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 23