Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 15:15-25 Biblia Habari Njema (BHN)

15. Matendo mengine yote ya Shalumu na njama zake zote alizofanya, yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.

16. Menahemu alipokuwa njiani kutoka Tirza, aliuharibu kabisa mji wa Tapua na kuangamiza wakazi wake pamoja na nchi yote iliyozunguka kwa sababu hawakujisalimisha kwake. Isitoshe, aliwatumbua wanawake waja wazito wote.

17. Katika mwaka wa thelathini na tisa wa enzi ya mfalme Azaria wa Yuda, Menahemu mwana wa Gadi alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa muda wa miaka kumi.

18. Alimwasi Mwenyezi-Mungu siku zote za utawala wala hakuacha maovu ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwapotosha watu wa Israeli wakatenda dhambi.

19. Basi, Pulu mfalme wa Ashuru, aliivamia Israeli, naye Menahemu akampa kilo thelathini na nne za fedha ili amsaidie kuimarisha mamlaka yake juu ya nchi ya Israeli.

20. Menahemu alipata fedha hiyo kwa kuwalazimisha matajiri wa Israeli kutoa mchango wa shekeli hamsini za fedha kila mmoja. Halafu Pulu hakukaa Israeli bali alirudi katika nchi yake.

21. Matendo mengine yote ya Menahemu yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.

22. Menahemu alifariki, naye mwanawe Pekahia alitawala mahali pake.

23. Katika mwaka wa hamsini wa enzi ya mfalme Azaria wa Yuda, Pekahia mwana wa Menahemu alianza kutawala Israeli, akatawala huko Samaria kwa muda wa miaka miwili.

24. Alimwasi Mwenyezi-Mungu na kufuata mfano mbaya wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, ambaye aliwafanya watu wa Israeli watende dhambi.

25. Peka mwana wa Remalia, ambaye alikuwa ofisa wa jeshi la Pekahia, alishirikiana na watu wengine hamsini kutoka Gileadi, akamuua Pekahia katika ngome ya ndani ya nyumba ya mfalme huko Samaria, na kuwa mfalme mahali pake.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 15