Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 13:1-10 Biblia Habari Njema (BHN)

1. Katika mwaka wa ishirini na tatu wa enzi ya mfalme Yoashi wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala Israeli, akaendelea kutawala huko Samaria muda wa miaka kumi na saba.

2. Alitenda dhambi mbele ya Mwenyezi-Mungu kama vile mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati aliyewakosesha watu wa Israeli wakatenda dhambi. Yehoahazi hakuacha matendo hayo mabaya.

3. Mwenyezi-Mungu alikasirika, akawafanya watu wa Israeli washindwe vitani mara kwa mara na mfalme Hazaeli wa Aramu na mwanawe Ben-hadadi.

4. Yehoahazi akamsihi Mwenyezi-Mungu, naye Mwenyezi-Mungu alipoona jinsi mfalme wa Aramu alivyowadhulumu watu wa Israeli alisikia maombi yake.

5. (Mwenyezi-Mungu akawapa watu wa Israeli kiongozi ambaye aliwakomboa kutoka kwa Washamu, ndipo wakakaa kwa amani kama vile walivyokuwa hapo awali.

6. Hata hivyo hawakuacha kutenda dhambi ambazo mfalme Yeroboamu aliwakosesha watu wa Israeli; lakini waliendelea na dhambi zao na sanamu ya mungu wa kike Ashera ilihifadhiwa huko Samaria.)

7. Yehoahazi hakuwa na majeshi, ila tu wapandafarasi hamsini, magari kumi na askari wa miguu 10,000. Hii ilikuwa ni kwa sababu mfalme wa Aramu alikuwa ameyaangamiza majeshi ya Israeli na kuyakanyaga chini kama mavumbi.

8. Matendo mengine yote ya Yehoahazi na ushujaa wake yameandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Nyakati za Wafalme wa Israeli.

9. Yehoahazi alifariki na kuzikwa huko Samaria, naye mwanawe Yehoashi akawa mfalme mahali pake.

10. Katika mwaka wa thelathini na saba wa enzi ya mfalme Yoashi wa Yuda, Yehoashi mwanawe Yehoahazi, alianza kutawala Israeli huko Samaria, na enzi yake ikaendelea kwa miaka kumi na sita.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 13