Agano la Kale

Agano Jipya

2 Wafalme 10:18-33 Biblia Habari Njema (BHN)

18. Yehu akawakusanya watu wa Samaria na kuwaambia, “Mfalme Ahabu alimtumikia Baali kidogo tu, lakini mimi nitamtumikia zaidi.

19. Waite manabii wote wa Baali, wafuasi wake wote na makuhani. Ni sharti kila mmoja afike, kwani nataka kumtolea Baali tambiko kubwa, na yeyote atakayekosa kufika atauawa.” Hiyo ilikuwa ni njama ya Yehu ili apate kuwaua wafuasi wa Baali.

20. Yehu akaamuru: “Alika mkutano mkubwa wa ibada ya Baali!” Tangazo likatolewa,

21. na Yehu akapeleka habari katika nchi yote ya Israeli ili wafuasi wote wa Baali wahudhurie kila mmoja. Wakaja wote na kujaa katika hekalu la Baali kutoka pembe moja mpaka nyingine.

22. Ndipo Yehu akamwagiza aliyesimamia mavazi matakatifu akisema, “Toa mavazi hayo na kuwapa watu waliohudhuria ibada.” Msimamizi akatoa mavazi hayo, akawapa.

23. Halafu Yehu akaingia katika hekalu la Baali akifuatana na Yehonadabu na kuwaambia waliokuwa hekaluni, “Hakikisheni kwamba waliomo hekaluni ni wale wamwabuduo Baali tu, na kwamba hakuna mtu yeyote anayemwabudu Mwenyezi-Mungu.

24. Kisha akaingia pamoja na Yehonadabu kumtolea Baali matambiko na tambiko za kuteketezwa. Yehu alikuwa ameweka watu themanini nje ya hekalu na kuwapa maagizo haya: ‘Waueni watu hawa wote. Yeyote atakayemwacha hata mmoja wao atoroke atalipa kwa maisha yake!’”

25. Mara Yehu alipomaliza kutoa tambiko ya kuteketezwa, aliwaambia walinzi na maofisa, “Ingieni mkawaue wote. Msimwache hata mmoja atoroke!” Wakaingia na panga zao tayari na kuwaua wote, kisha wakatoa maiti zao nje. Ndipo wakaingia chumba cha ndani cha hekalu,

26. na kutoa nguzo takatifu na kuiteketeza kwa moto.

27. Wakaharibu nguzo pamoja na hekalu; wakaligeuza hekalu kuwa choo; na hivyo ndivyo ilivyo mpaka hivi leo.

28. Hivyo ndivyo Yehu alivyofuta ibada za Baali katika Israeli.

29. Lakini alifuata dhambi ya Yeroboamu mwana wa Nebati ya kuwaongoza Waisraeli watende dhambi. Aliweka sanamu za ndama wa dhahabu huko Betheli na Dani.

30. Mwenyezi-Mungu akamwambia Yehu, “Umewatendea wazawa wa Ahabu yale yote niliyotaka uwatendee. Kwa hiyo nimekuahidi kuwa wazawa wako hadi kizazi cha nne watatawala Israeli.”

31. Lakini Yehu hakutii sheria za Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, kwa moyo wake wote. Badala yake, alifuata mfano wa Yeroboamu aliyewapotosha watu wa Israeli wakatenda dhambi.

32. Wakati huo Mwenyezi-Mungu alianza kupunguza eneo la nchi ya Israeli. Mfalme Hazaeli wa Aramu akashinda nchi yote ya Israeli,

33. kutoka upande wa mashariki ya mto Yordani, na nchi za Gileadi, Gadi, Reubeni na Manase na kutoka Aroeri ulioko kwenye bonde la Arnoni, kwenye nchi za Gileadi na Bashani.

Kusoma sura kamili 2 Wafalme 10