Agano la Kale

Agano Jipya

2 Samueli 9:6-13 Biblia Habari Njema (BHN)

6. Basi, Mefiboshethi mwana wa Yonathani, na mjukuu wa Shauli akaenda kwa mfalme Daudi, akaanguka kifudifudi mbele ya mfalme Daudi, akasujudu. Daudi akamwita, “Mefiboshethi.” Naye akamjibu, “Naam! Mimi hapa mtumishi wako.”

7. Daudi akamwambia, “Usiogope. Mimi nitakutendea wema kwa ajili ya baba yako Yonathani. Ile ardhi yote iliyokuwa ya babu yako Shauli nitakurudishia. Nawe, daima utakula mezani pangu.”

8. Mefiboshethi akasujudu, na kusema, “Mimi ni sawa na mbwa mfu; kwa nini unishughulikie hivyo?”

9. Kisha, mfalme Daudi akamwita Siba mtumishi wa Shauli, akamwambia, “Ile mali yote iliyokuwa ya Shauli na jamaa yake nimempa mjukuu wa bwana wako.

10. Wewe, watoto wako na watumishi wako mtakuwa mnamlimia Mefiboshethi na mtamletea mavuno ili mjukuu wa bwana wako awe daima na chakula. Lakini yeye atakula mezani pangu.” Wakati huo, Siba alikuwa na watoto wa kiume kumi na watano na watumishi ishirini.

11. Kisha, Siba akamwambia mfalme, “Mimi mtumishi wako, nitafanya yote kulingana na amri yako.” Basi, Mefiboshethi akawa anapata chakula chake mezani pa Daudi, kama mmojawapo wa watoto wa mfalme.

12. Mefiboshethi alikuwa na mtoto mdogo wa kiume aliyeitwa Mika. Watu wote wa jamaa ya Siba wakawa watumishi wa Mefiboshethi.

13. Hivyo, Mefiboshethi aliyekuwa amelemaa miguu yake yote akawa anaishi mjini Yerusalemu, na kupata chakula chake mezani pa mfalme daima.

Kusoma sura kamili 2 Samueli 9